Na mwandishi wetu
MBUNGE mteule wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, amesema ushindi wa kishindo wa Dk. John Magufuli, ni ishara kuwa watanzania wanataka mabadiliko ya maendeleo na si bora mabadiliko.
Amesema ana imani kubwa watanzania hawatajutia uamuzi wala kura zao walizompigia Dk. Magufuli kwa kuwa, yote aliyoahidi yanakwenda kufanyiwa kazi na hatimaye Tanzania kuwa ya tofauti katika muda mfupi ujao.
Aidha, amesema uchaguzi umemalizika kwa amani na watanzania wamefanya uamuzi sahihi hivyo, kilichobaki ni wote kuungana na kufanya kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko yanayokusidiwa.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoa shukrani zake kwa Watanzania na wananchi wa Singida kwa kumchagua Dk. Magufuli na wagombea ubunge na udiwani wa CCM.
Alisema wananchi wa Singida wameonyesha mshikamano mkubwa na ukomavu wa kisiasa kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya hadhara kusikiliza sera na baadaye kufanya uamujzi sahihi wa kuwachagua kwa kishindo wagombea wa CCM.
“Niko hapa kuwashukuru Watanzania wote kwa kufanya uamuzi sahihi wa kumchagua mgombea urais wetu, Dk. John Magufuli kwa kishindo na hatimaye kutangazwa kuwa mshindi.
“Uamuzi waliofanya umetokana na CCM kusimamisha mtu makini, mwadilifu na mwenye dhamira ya dhati ya kutuletea maendeleo ya haraka na ya kweli. Kazi kubwa iliyopo mbele yetu ni kuungana na kufanya kazi kwa bidii kutimiza ndoto za watanzania. Falsafa yetu ya HapaKaziTu ndiyo inakwenda kutekelezwa sasa,” alisema Aysharose.
Mbunge huyo mteule, ambaye amejizolea sifa na umaarufu mkubwa kutokana na kupambana kikamilifu katika kusaka ushindi wa wagombea wa CCM katika ngazi ya utais, ubunge na madiwani, alisema amejipanga kuhakikisha anatatua changamoto zinazowakabili wanawake na vijana.
Alisema wakati wa kampeni, alizunguka katika maeneo mbalimbali mkoani Singida na huko alikutana na kero mbalimbali ambazo tayari ameanza kuzifanyia kazi kabla ya kuwapishwa kuwa mbunge.
Aysharose alisema changamoto ya huduma za afya na uwezeshaji kiuchumi kwa akinamama na vijana ndiyo kitakuwa kipaumbele chake cha kwanza mara baada ya kuapishwa.
“Nimeona changamoto nyingi, lakini kwa kuanzia nitaweka nguvu katika huduma za afya na uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake ili kuwawezesha kukua kiuchumi. Natambua kuwa ukimuwezesha mwanamke basi umewezesha familia nzima kusonga mbele kimaendeleo na hili, nitalipa msukumo wa aina yake,” alisema.
No comments:
Post a Comment