Saturday, September 26, 2015

Salam za Eid na Rambirambi kutoka kwa Zanzibar Diaspora (ZADIA)


                            TAARIFA
Assalamu Alaykum: Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Allah Subhanahu Wa Taala kwa kutujaalia kuwa wazima na kuadhimisha Siku Kuu ya Idd Al-Adh-ha ya mwaka 1436H (2015). 
Idd Al-Adh'ha ni Siku Kuu kubwa kati ya Siku Kuu mbili katika Uislamu, ni siku ya furaha, kwa familia na jamii kwa ujumla. Kwa niaba ya Uongozi wenu wa ZADIA, naungana na WanaZadia wote, Wazanzibari, na Waislamu kwa ujumla katika kuadhimisha siku hii adhimu.
Kwa vile hii ni Siku Kuu Kubwa, furaha yangu ingekuwa kubwa zaidi katika kusherehekea. Hata hivyo, furaha hiyo imeingia doa kutokana na maafa yaliyowakumba ndugu zetu Waislamu waliofunga safari kwenda kuhiji, kuitikia wito wa Mola Wao Mlezi wa kuizuru Nyumba Yake
Tukufu.
Kutokana na hilo, napenda kuchukua fursa hii kutoa salamu zangu za rambirambi kwa Waislamu wote ulimwenguni ambao wamepoteza ndugu, jamaa na marafiki katika maafa hayo.
Tunamuomba Allah awaingize wenzetu waliotangulia peponi kwa Rehma zake. Kama ambavyo, natoa pole kwa Mahujaji wote waliopata ajali na kujeruhiwa, na kumwomba Allah SWT awape afya na uzima na kuwarejea katika familia zao wakiwa katika afya na uzima.
Ndugu Wanazadia na Wazalendo kwa ujumla,
Huku tukiwa tunaendelea kusherehekea Siku Kuu ya Idd Al-Adh'ha, napenda kuwakumbusha kuhusu majukumu ya kila mmoja wetu ya kuendeleza umoja, mshikamano na amani katika Jumuiya yetu na nchi yetu Zanzibar kwa ujumla. Na hakuna njia nyepesi ya kufikia malengo hayo ispokuwa kushikamana na Kamba ya Mwenyezi Mungu.
Tujifunze kutokana na somo la Hijja ambalo Waislamu kutoka sehemu zote duniani hukutan sehemu moja wakiwa katika vazi la aina moja kwa ajili ya kuabudu Mola mmoja, bila kujali kabila, nchi wanazotoka, umri, jinsia, vyeo au tofauti nyenginezo. Wote wako sawa wakiwa na lengo moja.
Siku Kuu hii kwa mwaka huu inakuja ikiwa imebakia si zaidi ya mwezi mmoja kabla Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuingia katika Uchaguzi Mkuu. Mara tu baada ya kumalizika kwa shamra-shamra za Siku Kuu, akili, macho na masikio yetu yote yataelekea kwenye kampeni za uchaguzi na vioja vyake.
Kwa hivyo, nasaha kwetu sote, wadau wote, kulitumia funzo tulilolipata katika Hijja na Siku Kuu yake kuhakikisha kuwa tunashiriki kwa njia moja au nyengine kuufanya uchaguzi ujao upite kwa salama na amani kama ulivyopita ule uliotangulia wa mwaka 2010.

 Tukumbuke kuwa Umoja ni nguvu na Utengano ni Udhaifu. Kwa hivyo, kampeni na ushabiki wetu wa kisiasa vyote vilenge kwenye kuendeleza Serikali ya Umoja Wa Kitaifa Zanzibar na kuipa nguvu Zanzibar kuleta maendeleo.
Ikumbukwe kuwa, Malengo Makuu ya ZADIA ni kuleta umoja wa Wazanzibari na Maendeleo yao nje na ndani ya nchi yetu tuipendayo. Hata hivyo, malengo hayo hayawezi kufikiwa bila kuwa na amani, usalama na utulivu ndani ya nchi yetu ya Zanzibar na hata Jamhuri yote ya Muungano wa Tanzania.
Kila mmoja wetu ajaribu kuyalinda malengo hayo kwa kuzingatia kauli ya Bwana Mtume SAW aliposema: "Kila mmoja wenu ni mchunga, na kila mmoja wenu ataulizwa juu ya kile anachokichunga".
Nawatakia Idi Njema, nawapa pole wafiwa na nawaombea majeruhi shifaa.
Omar H. Ali,
Mwenyekiti,
ZADIA.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...