Monday, October 02, 2017

Zawadi za milioni 40 kushindaniwa Rock City Marathon

Washindi wa michuano ya Rock City Marathon inayotarajiwa kufanyika  Octoba 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wanatarajiwa kuondoka na zawadi zenye thamani ya zaidi ya sh milioni 40 pamoja na medali, imefahamika. 


Akizungumzia zawadi hizo jijini Dar es Salaam leo, Mratibu wa mbio hizo kutoka kampuni ya Capital Plus International (CPI), Bw. Bidan Lugoe  alisema pamoja na medali washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 42 kwa wanaume na wanawake watajinyakulia sh. Mil 4 kila mmoja, sh.mil 2/-  kwa washindi wa pili na sh. Mil 1/- kwa washindi wa tatu, huku washindi wanne hadi kumi na tano nao pia wakiibuka na zawadi  za medali na pesa taslimu.


Kwa upande wa mbio za  Kilomita 21, Bidan alisema pamoja na medali washindi wa kwanza kwa wanaume na wanawake watajinyakulia sh.  Mil 2/- kila mmoja, sh. Mil 1/-  kwa washindi wa pili na sh. Laki 5/- kwa washindi wa tatu huku pia washindi wanne hadi wa kumi na tano wakiibuka na  zawadi za pesa taslimu na medali kila mmoja.


 “Mbio za kilomita tano tunatarajia kwamba zitaongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe, baadhi ya wakuu wa mikoa kutoka kanda ya Ziwa huku pia zikihusisha wadhamini wa mbio hizi kutoka mashirika mbalimabli yaani(Corporates).’’ Alisema.


Aidha wadhamini ambao pia watashiriki katika mbio hizo ni pamoja na kampuni za Tiper, Puma Energy, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, New Mwanza Hotel, Real PR Solutions, Efm Radio, EF Out Door, CF Hospital na Afrimax Strategic Partnerships Limited.



Alibainisha kuwa mbio hizo za Km 5 zitahusisha watu wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino ambapo washindi kwa upande wa mashirika watapatiwa zawadi za utambuzi ikiwemo medali na vyeti vya ushiriki huku pesa zikielekezwa kwa washiriki wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino.


Alisema washindi wa mbio za Kilomita tatu ambazo zipo mahususi kwa ajili ya wazee watapatiwa sh 100,000/- kwa washindi wa kwanza huku washindi wa pili wakipata sh 70,000/ na watatu  wakipatiwa sh 50,000/-pesa taslimu.


 “Kwa washindi wa mbio za kilomita mbili na nusu zitakazohusisha watoto wenye umri kati ya miaka 7 hadi 10 watapatiwa sh 50,000/-kila mmoja huku wa pili na watatu pia wakipatiwa pesa taslimu.’’ Aliongeza


Zaidi aliongeza kwamba washindi kwanza kwenye  mbio fupi za uwanjani  za mita 100,200,  400, 800 na 1500 ambazo ni mahususi kwa wanafunzi watapatiwa zawadi ya sh 50,000/ kila mmoja (wanaume na wanawake), sh 30,000 kwa washindi wa pili huku washindi watatu wakiambulia kiasi cha sh 20,000 kwa kila mmoja.


Akizungumzia usajili wa mbio hizo Bw. Bidan alisema kwa wakazi wa jiji la Mwanza na mikoa jirani wanaweza kujisajili kwa kuchukua fomu katika vituo kadhaa vikiwemo Ofisi za michezo wilaya zote za mkoa wa Mwanza, Ofisi zote za riadha mikoa ya Geita, Simiyu na Shinyanga,   Uwanja wa Nyamagana,  Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino  Mwanza, Kituo cha michezo  Malya, Shule ya Kimataifa ya Isamilo, New Mwanza  Hotel na Ofisi za EF Out door zilizopo jingo la Rock City Mall.


“Kwa upande wa Dar es Salaam Fomu za ushiriki pia zinapatikana katika ofisi za Kampuni ya Capital Plus International zilizopo ghorofa ya sita jengo la SHAMO Tower, Mbezi Beach , jijini Dar es, Salaam na EFM Jogging Club iliyopo Coco Beach  Dar es Salaam” alitaja.


Zaidi kuhusu usajili wa mbio hizo zinazoandaliwa kwa kushirikiana na Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza (MWAA), Bidan alisema unaweza kufanyika kupitia tovuti ya kampuni hiyo ambayo ni www.capitalplus.co.tz


Alitoa wito kwa washiriki zaidi kujisajili ili kuthibitisha ushiriki wao kwenye mbio hizo ambazo mbali na kuibua vipaji vya mchezo wa riadha hapa nchini pia zinalenga  kupambana na ujangili pamoja na kutangaza utalii katika mikoa iliyopo Ziwa ya Ziwa.


No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...