Tuesday, October 03, 2017

WAZIRI MBARAWA: WAKANDARASI JENGENI BARABARA KWA VIWANGO



Serikali imesema itahakikisha inaendelea kuwasimamia wakandarasi wa Ujenzi wa Barabara kuhakikisha wanajenga barabara zote nchini kwa viwango vilivyokusudiwa na kumaliza kwa wakati ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa leo jijini Dar es salaam mara baada ya kukagua Awamu ya Tatu ya utekelezaji wa Ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano jijini humo ambapo ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wake na kusisitiza kwa Wakala wa Baraba (TANROADS), mkoa wa Dar es salaam kuwa wakali katika usimamizi ili kuhakikisha barabara hizo zinajengwa kwa viwango vilivyokubaliwa kwenye mkataba.

“ Serikali imekuwa ikitumia Fedha nyingi katika kutekeleza miradi hii, hivyo TANROADS hakikisheni mnasimamia wakandarasi hawa kujenga barabara hizi kwa viwango na kwa wakati”, amesema Waziri Mbarawa.

Aidha, Waziri Mbarawa amefafanua kuwa utekelezaji wa awamu hiyo unaendelea vizuri ambapo unahusisha barabara ya Kifuru – Msigani (km 4.5) ambayo kwa sasa imefika asilimia 87, Goba – Makongo (km 4.5), nayo imefikia asilimia 52 na Goba – Madale (km 5) yenye asilimia 5.

Profesa Mbarawa ametoa wito kwa wananchi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi naTANROADS mkoa wa Dar es salaam wakati mradi huo ukiendeleaa kutekelezwa ili kusaidia kumaliza kwa wakati.

Waziri Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kushughulikia suala la ulipaji wa fidia kwa wananchi wa maeneo hayo ambao wamepitiwa na mradi huo. Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Dar es salaam, Mhandisi Julius Ndyamkama, amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa watasimamia mradi huo usiku na mchana ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyo bora.

Mhandisi Ndyamkama amebainisha changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa mradi huo ikiwemo suala la ulipaji wa fidia kwa baadhi ya maeneo hasa katika kipande cha barabara chenye urefu wa kilometa 1 kuanzia Mto Mbezi kuelekea Makongo.

Naye, Mratibu wa Mradi wa barabara ya Goba – Madale (km 5), kutoka kampuni ya Ujenzi ya Mwananchi Engineering and Contracting Co. Ltd (MECCO), Mhandisi Crispin Mwombeki, amesema kuwa tayari wameshakamilisha usanifu wa mradi na wanategemea kuanza kazi za Ujenzi hivi karibuni.

Utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya mradi wa Ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano katika jiji la Dar es salaam umeanza mwezi Desemba, mwaka 2016 ambapo umehusisha barabara tatu za Kifuru – Msigani (km 4.5), Goba – Makongo (km 4.5), na Goba – Madale (km 5) na kugharimu Jumla ya Shilingi Bilioni 24.2.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...