Tuesday, October 31, 2017

Waziri Mwakyembe azindua Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ya kupata Uhuru

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amezindua Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ambayo yanalenga kuonyesha namna mashujaa wa Tanganyika walipambana kupata uhuru, maonyesho ambayo yatafanyika kwa muda wa mwezi mmoja katika Makumbusho ya Taifa- Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam. Uzinduzi wa maonyesho hayo ambao ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), kwa lengo ya kuendeleza juhudi za Uhifadhi wa Hifadhi ya Urithi Tanzania,hususani ya Ukombozi wa Afrika yanasimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa maonyesho hayo, Dkt. Mwakyembe alisema mradi huo wa kuhifadhi historia ya Ukombozi wa bara la Afrika ni muhimu kwa Tanzania kwani unaweza kusaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini kuliko ilivyo sasa kwani inawapa nafasi wageni ya kuona mambo tofauti na yaliyozoeleka pindi wanapokuja nchini. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ya kupata Uhuru. “Tuna mradi ambao utatupeleka mbali sana Watanzania, Afrika Kusini, Namibia, Angola hata wao wametuambia tusije shangaa sehemu hiyo ikawa inaleta watalii wengi zaidi kuliko wanaokuja kuangalia tembo na simba, urithi wa Afrika tumekabidhiwa na bara la Afrika ni wajibu wetu Watanzania kuusukuma huu mradi maana tumeshachelewa, Watanzania wengi labda hawaelewi mwaka 2011 kwa kushirikiana na UNESCO tulipeleka ombi AU la mradi huu wa bara la Afrika na wakaubariki huu mradi na wakaamua makao makuu yawe Tanzania na sisi tukachagua Dar na hapa kitajengwa kituo kikubwa kitakuwa na historia ya Ukombozi wa Afrika, sisi ndiyo viongozi wa huu mradi,” alisema Dkt. Mwakyembe. Alisema ili kufanikisha mradi huo tayari wameanza kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha pindi watakapojenga kituoambacho kitatumika kuhifadhi vitu mbalimbali ambavyo vilitumika katika kipindi cha ukombozi wa bara la Afrika kuwe na taarifa nyingi kuhusu bara la Afrika. “Tunawatumia wazee walio na historia ya ukombozi wa Afrika tumehoji zaidi ya wazee 100 na tunaendelea na hilo zoezi na tumebaini maeneo zaidi ya 200 Tanzania ambayo yanahitaji kuhifadhiwa, ni wajibu wangu kupeleka muswada bungeni ili tuyahifadhi na kuyalinda kwa kutumia sheria,” alisema Waziri Mwakyembe. Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini (EU), Roeland Van de Geer akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ya kupata Uhuru. Kwa upande wa Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini (EU), Roeland Van de Geer alisema ni muhimu kwa bara la Afrika kuwa na maonyesho ambayo yanaelezea historia ya bara hilo ili yatumike kuelezea kizazi cha sasa na kijacho namna nchi za Afrika zilipambana kupata uhuru na wao kama EU wataendelea kusaidia miradi mbalimbali yenye lengo ya kutunza urithi wa bara la Afrika. “Ni jambo la kujivunia kwa Umoja wa nchi za Ulaya kusaidia kufanikisha mradi huu … EU tumekuwa tukisaidia miradi mingi na hii yote ni kwa ajili ya kutunza utamaduni na urithi wa bara la Afrika, tumesaidia miradi mbalimbali nchini ikiwepo ya Olduvai na Ngorongoro na tutaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania kuendeleza maeneo ya kihistoria,” alisema. Afisa Mpango Kitaifa wa UNESCO, Nancy Kaizilege akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ya kupata Uhuru. Naye Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO kanda ya Afrika Mashariki na Afisa Mwakilishi wa Unesco Dar, Ann Therese Ndong- Jatta katika hotuba yake iliyosomwa na Afisa Mpango Kitaifa wa UNESCO, Nancy Kaizilege alisema ni jambo zuri kuwepo na makumbusho ambayo yanaeleza historia ya bara la Afrika na yatawza kuwapa nafasi watu mbalimbali kutoka mataifa ya nje ya bara la Afrika kuona na kujifunza historia ya Afrika. “Makumbusho haya ni muhimu kwasababu ni sehemu ya ukumbusho wetu kwa baadae, kupitia makumbusho haya tutaona historia ya bara la Afrika, historia ya mwanadamu na safari ya kutafuta uhuru ilivyokuwa,” alisema Kaizilege. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe na Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini (EU), Roeland Van de Geer wakikata utepe katika uzinduzi wa Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ya kupata Uhuru.Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa ameongozana na Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini (EU), Roeland Van de Geer na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuangalia vitu mbalimbali vya kihistoria ambavyo vimewekwa katikaMaonyesho ya Mashujaa na Mapambano ya kupata Uhuru.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...