Tuesday, October 03, 2017

PPF YATOA MSAADA WA VIFAA VYA MAABARA

 Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio akikabidhi moja ya Vifaa vya maabara kwa mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Canossa Mhandisi Magayane Machibya wakati wa mahafali ya tisa ya ka kidato cha nne Jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, William Erio (Kulia) akimkabidhi cheti Joyce Msumari (Kushoto) mhitimu wa kidato cha Nne katika shule ya Sekondari ya Wasichana ya Canossa iliyopo jijini Dar es Salaam.  Joyce Msumari ni mmoja wa wanufaika wa Fao la Elimu linalotolewa na PPF kwa watoto wa wananchama wanaofariki wakiwa katika Ajira.  
 Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Canossa, Mhandisi Magayane Machibya (Kushoto) na Mkuu wa Shule hiyo Sista Irene Natumanya wakifurahia kupokea vifaa vya maabara kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa PPF William Erio (hayupo pichani) 
 Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Canossa Sista Irene Natumanya (Kulia) akimpa mkono wa shukrani Mkurugenzi Mkuu wa PPF Bwana William Erio (Katikati) baada ya kukabidhiwa vifaa vya maabara na Mfuko wa PPF mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Mkurugenzi wa Bodi ya Shule hiyo Mhandisi Machibya Magayane.
 Wahitimu wa Kidato cha nne wa shule ya Sekondari ya Canossa wakitumbuiza katika mahafali ya 9 yaliofanyika Shuleni hapo mwishoni mwa wiki.
Vifaa vya maabara vilivyotolewa na Mfuko wa Pensheni wa PPF wakati wa mahafali ya 9 ya shule ya Sekondari ya Wasichana Canossa mwishoni mwa wiki.

MFUKO wa Pensheni wa PPF umetoa msaada wa vifaa vya maabara vyenye thamani ya zaidi ya shillingi milioni 6.7 kwa shule ya Sekondari ya Wasichana ya Canossa iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam.

Akikabidhi vifaa hivyo katika mahafali ya tisa ya kidato cha nne shuleni mwishoni mwa wiki,Mkurugenzi Mkuu wa PPF Bw.William Erio amesema Mfuko umeamua kutoa vifaa hivyo ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano katika kutengeneza uchumi wa viwanda.

Bw.Erio ambaye pia alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo, amebainisha kuwa Mfuko wa Pensheni wa PPF utaendelea kushirikiana na taasisi za elimu nchini katika jitihada za kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Pia Bw.Erio amesema ushirikiano mzuri uliopo kati ya shule ya Canossa na PPF pia ni moja ya sababu kupeleka vifaa hivyo shuleni hapo..

“Shule ya Canossa imekuwa miongoni mwa waajiri wanaowasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati bila kuchelewesha,na idadi kubwa ya wafanyakazi wake ni wanachama wa Mfuko wetu,” amefafanua Mkurugenzi Mkuu.

Sanjari na hilo, Mkurugenzi huyo wa PPF amesema katika shule hiyo Mfuko umeshasomesha wanafunzi 6 ambao wamenufaika na fao la elimu baada ya wazazi wao ambao walikuwa wanachama wa PPF kufariki wakiwa katika ajira.

“Mfuko pia unabeba jukumu la mzazi, kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2017, tumesomesha wanafunzi 1403 nchi nzima na zaidi ya shilingi 1.4 bilioni zimetumika katika kugharamia masomo yao’’. 

Mmoja wa wahitimu ambaye pia ni miongoni mwa wanafunzi wanaosomeshwa na Mfuko wa PPF, Joyce Msumari ameshukuru PPF kwa kumlipia masomo yake tangu mzazi wake alipofariki  akiwa darasa la tano, miaka 7 iliyopita.

“Naishukuru PPF kwa kunifikisha hapa,na wazazi wengine wanaweza kujifunza kupitia kwangu maana hakuna anayeijua kesho yake hivyo unapojiunga na Mfuko huu utakuwa na uhakika wa masomo kwa mwanao pale ambapo Mungu ataamua kukuchukua na kuwaacha watoto wako wakiwa wanahitaji,” alisema mwanafunzi huyo.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...