Wednesday, October 25, 2017

WAZIRI MHAGAMA AIPONGEZA PUMA KUBORESHA HALI ZA WAFANYAKAZI, ATAKA WAAJIRI WENGINE WAIGE

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Kazi, Ajira,Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama (katikati) akifurahia kitendo cha Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uuzaji Mafuta ya Puma, Philippe Corsaletti (kushoto) akibadilishana hati za mkataba  wa hiari uboreshaji hali bora za Wafanyakazi wa kampuni hiyo na Mkuu wa  Kitengo cha Biashara cha TUICO, Jonathan Peres wakati wa hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Puma, Dar es Salaam leo.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama (katikati) akishuhudia  Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uuzaji Mafuta ya Puma Energy, Philippe Corsaletti (kushoto) na Mkuu wa  Kitengo cha Biashara cha TUICO, Jonathan Peres wakitiliana saini mkataba  wa hiari uboreshaji hali bora za Wafanyakazi wa kampuni hiyo wakati wa hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Puma, Dar es Salaam leo.
 Baadhi ya Wafanyakazi na wanahabari wakishuhudia tukio hilo

 Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Kampuni ya Puma, Raymond Tungaraza akitoa shukrani kwa Uongozi wa Puma kwa kukubali mabrosho hayo kwa wafanyakazi ambao hivi sasa kima cha chini kitaanzia sh. mil. 1, Puma italipia ada za watoto wa wafanyakazi sh. 900 Shule ya msingi,  Mil. 1.2 Sekondari na Mil. 1.5 sekondari pia inawalipia wafanyakazi Bima ya Maisha.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama (katikati) akizungumza jambo na   Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uuzaji Mafuta ya Puma, Philippe Corsaletti.





 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama akihutubia wakati wa hafla hiyo, ambapo aliagiza waajiri wote kuiga mfano wa Puma kwa kuingia mikataba ya hiari na wafanyakazi.

 Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Aggrey Mlimuka akizungumza wakati wa hafla hiyo
Meneja Rasilimali Watu wa Puma, Loveness Hoyange akielezea kwa ufupi kuhusu makubaliano ya mkataba huo


Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Puma Energy Tanzania, imetiliana sahihi mkataba wa hiari kati yake na Chama cha wafanyakazi Tanzania (Tuico) huku Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge,Kazi,Vijana, Ajira na Walemavu), Jenista Mhagama akipongeza hatua hiyo na kuzitaka kampuni zingine kuiga mfano huo.

Akasisitiza kuwa Kampuni ya Puma kutokana hatua hiyo na historia yao kati ya uongozi na wafanyakazi, ameridhika na namna ambavyo wanashirikiana katika masuala ya kulinda maslahi kazini.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam jana Makao Makuu ya Puma Energy Tanzania, Waziri Mhagama alisema kampuni hiyo ameiondoa kwenye orodha ya kampuni zenye migogoro kati ya menejimenti na wafanyakazi.

“Puma mnastahili pongezi kwa hatua hii ambayo mmeifanya, kwetu Serikali tumefarijika sana na tunaunga mkono juhudi hizi.Pia nasi ni sehemu ya kampuni hii kutokana na umiliki wa hisia wa asilimia 50 kwa 50, hivyo kila mnachokianya na kuleta mafanikio nasi serikali ni sehemu ya ufanikishaji huo.

“Tunaamini kwa maboresho ambayo mmeyafanya kwenye kuangalia maslahi ya wafanyakazi wenu ni jambo muhimu na jema kwa nchi yetu.Tunaamini wakanyakazi wakiwa salama kazini na kupata stahiki zao inaleta tija na ufanisi na matokeo uchumi wa nchi kukua,”alisema Waziri Mhagama.

Aliisifu pia hatua ya kwamba kampuni hiyo imefikia makubaliano kati yake na wafanyakazi kuwa kuanzia mwakani  kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wake kitakuwa Sh. milioni moja huku pia ikilipa ada za shule  ya msingi, sekondari na Chuo Kikuu kwa wale ambao watakuwa  wakisomesha watoto zao katika shule hizo.

Alisema kwa niaba ya Serikali anakumbusha waajiri wote nchini kutafuta suluhu ya migogoro kwani anaamini kila kampuni, taasisi au shirika kuna vyama vya wafanyakazi na wanaoshindwa kufanya hivyo wanakiuka sheria za kazi.

Awali Meneja Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Philippe Corsaletti alisema wamefikia hatua hiyo muhimu katika uendeshaji wa shughuli zake hapa Tanzania kwa kufanya mapitio na kusaini mkataba wa hiari kati yake na chama cha wafanyakazi ambacho kiliwakilisha wafanyakazi.

“Mkataba huu wa leo unachukua nafasi ya ule uliokuwepo. Na ambao umebaki katika kutekelezwa kwa viwango vyote hadi sasa. 

“Jambo la muhimu sana la kufahamu ni kwamba kwa nyakati zote za makubaliano, mazungumzo yamekua yakifanyika katika hali ya utulivu, kuaminiana na katika mazingira rafiki,”alisema.  

Alifafanua makubaliano ya mwaka huu yametiwa sahihi na kushuhudiwa na Waziri Mhagama ambapo Puma Tanzania ilianza uwepo wake hapa Tanzania mwaka 2011 baada ya kuchukua hisa zilizokua zikimilikiwa na kampuni ya BP. 
Alisema kwa sasa kampuni inamilikiwa kwa pamoja kati ya Puma Group kwa asilimia 50 na Serikali ya Tanzania asilimia 50.


“Wafanyakazi wetu ndio moyo wa biashara yetu na ningependa kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa utendaji wao wa pekee na kujitoa pasipo kuchoka katika kuifanya Puma Energy kuwa kampuni ya kiwango cha kimataifa” alisema Corsaletti.

Alisema kampuni ya Puma inajivunia mahusiano maalumu na kuaminiana ambako kumejengeka kati ya wafanyakazi pamoja na chama ambako kumewezesha maboresho katika maeneo mbalimbali.

Alitaja baadhi ya maeneo hayo ni kuboresha mahusiano na wafanyakazi kupitia uwazi na kujifunga kwa kusaini mkataba wa hiari (CBA) ambapo tumeboresha baadhi ya mahitaji ya kisheria  ya sheria za kazi pamoja na kanuni zake.

Pia Puma Tanzania imekua moja ya kampuni zinazotimiza sheria pamoja na kanuni mahali pote tunapofanya kazi na mfano mwaka huu Puma imepewa tuzo kutoka PPF kwa kuwa mshindi wa pili katika kulipia wafanyakazi wake michango yao ya akiba.

Aliongeza Kuhakikisha wafanyakazi wake wanatenda kazi katika kiwango cha juu cha ubora katika masuala ya Afya usalama na mazingira na kutimiza viwango vya kimataifa vya usalama. 

“Kwa sasa Puma Tanzania ni kampuni pekee katika kampuni za mafuta ambayo imetimiza vigezo na kupewa cheti cha ubora wa bidhaa cha kimataifa (ISO 9001-2008) na cheti cha ubora wa mazingira cha kimataifa (ISO 14001-2004),”alisema.
Pia imejizatiti katika kuwaendeleza wafanyakazi wake kupitia mfumo wa mafunzo na uendelezaji kazini ambapo kampuni hutumia takribani Sh. milioni 200 kwa mwaka katika mafunzo na uendelezaji.

Eneo jingine Puma Tanzania pia imejizatiti katika kujenga uwezo na kutengeneza fursa kwa vijana kupitia mpango wake wa uendelezaji wa wahitimu wa vyuo vikuu ambapo kila mwaka tunaajiri hadi vijana watano na kuwabakisha wale wanaoonesha bidii katika utendaji.

“Mkataba wa hiari wa mwaka 2017 umeboresha mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuongeza ada za shule kwa ajili ya watoto wa wafanyakazi kuanzia shule za Msingi hadi Chuo Kikuu ambapo wafanyakazi wenye watoto wanapewa kiasi cha Sh 900,000 kwa shule za Msingi, Sh milioni 1.2 wa shule za sekondari,

“Na Sh. milioni 1.5 kwa vyuo vikuu. Malipo haya hulipwa moja kwa moja katika akaunti ya mfanyakazi kila mwezi Desemba ili kusaidia katika malipo ya ada za shule,”alisema.

Corsaletti alisema kuwa wameboresha Bima ya maisha pamoja na malipo yanayofanywa na mfuko wa serikali wa kulipa fidia kwa wafanyakazi na  utaratibu wa kampuni wa kutoa matibabu bure kwa wafanyakazi na familia zao, kila mfanyakazi anakatiwa bima ya  maisha kila mwaka ili kuisaidia familia endapo kutatokea kifo cha mfanyakazi akiwa kazini ambapo ni sawa na mshahara wa miaka mitatu.

“Kuongeza alawansi zaidi kwa wafanyakazi wanaofanya kazi nje ya muda kama vile malipo ya kuitwa kazini baada ya saa za kazi, malipo ya usiku n.k.

“Mwaka 2016, Puma Tanzania ilishinda tuzo kutoka katika umoja wa waajiri Tanzania (ATE) kama mwajiri bora katika kundi la mahusiano na wafanyakazi. Hii ni mfano mmoja tu kuonyesha namna ambavyo tumejizatiti katika kuimarisha mahusiano na wafanyakazi wetu.

“Tutaendelea kushirikiana bega kwa bega pamoja na wizara yako, chama cha waajiri, chama cha wafanyakazi, pamoja na wafanyakazi wetu katika kuhakikisha kwamba tunatengeneza mazingira tulivu ya kazi kwa watu wetu,”alisema  Corsaletti.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...