Tuesday, October 31, 2017

OFISI YA MAKAMU WA RAIS YAANDAA WARSHA YA UZINDUZI WA MRADI WA KUJENGA UWEZO KWA TAASISI KATIKA UDHIBITI WA KEMIKALI NA TAKA SUMU


 Mgeni Rasmi katika warsha ya uzinduzi wa Mradi wa kujenga uwezo kwa Tasisi katika udhibiti wa kemikali na taka sumu , Bwana Richard Muyungi ambaye ni Mkurugenzi idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais akiongeakatika uzinduzi wa warsha hiyo.
 Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais Bi Magdalena Mtenga akiongea wakati wa warsha hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, Idara ya Mazingira.
 Sehemu ya Washiriki wa warsha hiyo wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi (hayupo pichani).
Mwakilishi wa UNEP  Bibi Nalimi Sharma akiongea katika warsha hiyo, pembeni yake Mkurugenzi wa Mazingira Ofsis Ya Makamu wa Raisambaye  ni Mgeni Rasmi Bwana Richard Muyungi
 Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bwana Richard Muyungi akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe waliohudhuria warsha hiyo kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali.

Nchi zinazoendelea zinakabiliwa na changamoto katika suala zima la usimamizi na udhibiti wa kemikali na taka sumu. Taka sumu nyingi zimekua tishio kwa Wananchi hasa Wanawake na Watoto. 

Hayo yamesemwa na Mgeni Rasmi  ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais,  Bwana Richard Muyungi alipokua akifungua warsha ya uzinduzi wa mradi wa kujenga uelewa kwa Taasisi za Serikali katika udhibiti na usimamizi wa kemikali na taka sumu jijini Dar Es Salaam.

Pia ametoa shukrani kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) kwa msaada wa kifedha katika kuanzishwa kwa mradi huo, ameongeza pia  Wajumbe waliohudhuria warsha hiyo wakaitumie vema elimu watakayoipata katika sehemu zao za kazi ili kuongeza weledi na maarifa.

Akiongea katika warsha hiyo Mwakilishi kutoka UNEP Bi.Nalimi Sharma amesema amefurahi sana kuhushuria uzinduzi wa warsha ya mradi huo na kuona jitihada mbalimbali zinazochukuliwa katika suala zima la usimamizi na udhibiti wa kemikali na taka sumu. Ameongeza kuwa UNEP itaendelea kutoa msaada wa kifedha kwa kwa Ofisi ili kuendelea kuimarisha shughuli za usimamizi na udhibiti wa kemikali na taka sumu. 

MAKANDARASI KUKUTANA JIJINI DAR, KUJADILI MAENDELEO YA UKUAJI WA VIWANDA


 Mwenyekiti wa Chama cha Makandarasi Mhandisi Lawrence Mwakyambiki (katikati) akieleza jambo kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) katika utambulisho wa mkutano wa chama hicho utakaofanyika Novemba 17, 2017 Diamondi Jubilee Jijini Dar es Salaam,kulia ni Meneja Mauzo wa benki ya cba Bi.Kunenguda Dedede na kushoto ni Mkuu wa Masoko kutoka NMB Bi.Linda Teggisa.
Meneja Mauzo wa benki ya cba Bi.Kunenguda Dedede akieleza jambo kwa waandishi wa habari( hawapo pichani)  kuhusu mkutano wa makandarasi hapo novemba 17, 2017 katika ukumbi wa diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam, wa kwanza kushoto ni Mkuu wa masoko  kutoka NMB Bi.Linda Teggisa na Mwenyekiti wa Chama cha Makandarasi Mhandisi Lawrence Mwakyambiki.(Picha na Paschal Dotto-MAELEZO)

Na.Paschal Dotto-MAELEZO.
Chama cha Makandarasi (CATA) kinachounganisha wakandarasi wote nchini kinatarajia kukutana Novemba 17, 2017 kujadili kuhusu ukuaji wa viwanda nchini mkutano utakaofanyika katika ukumbi wa Diamondi Jubilee Jijini Dar es Salaam.

Akizungumuza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Mhandisi Lawrence Mwakyambiki alisema kuwa  Serikali ya Aawamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli iko kwenye njia ya ujenzi wa viwanda kwa hiyo sekta ya ujenzi inahitajika kwa kiasi kikubwa kwenye sera hii ya viwanda.

“Lengo la mkutano huu kwa wakandarasi hawa ni kutaka kuleta mchango wao katika ujenzi wa uchumi wa Tanzania na wameona kwamba kama wazawa wanaowajibu wa kutoa mchango katika katika ujenzi wa viwanda nchini”, alisema Mhandisi Mwakyambiki.

Aidha Mhandisi Mwakyambiki aliseka kuwa katika maendeleo ya taifa tasnia ya ujenzi ni muhimu kwani inabeba vitu vingi na kuwawezesha wananchi kupata huduma stahiki kama elimu na afya na kuwataka makandarasi kufanya kazi zo kwa ufanisi mkubwa.

Katika mkutano huu ambapo CATA watakuwa waratibu vyama vingine vya wakandaarasi vikiwemo Tanzania Civil Engineering Contractors Association(TACECA) pamoja na Association of Citizen Contractors(ACCT) na  mabenki  ya cba na NMB ambayo yatatoa ufadhili wa mkutano huo.

Akibainisha miradi itakayochukua nafasi katika majadiliano hayo Mwakyambiki alisema kuwa katika serikali hii ya awanu ya tano miradi inayohitaji  wakandarasi ni Ujenzi wa miundombinu ya reli(SGR), sekta ya maji, bomba la kusafirisha mafuta ghafi(uganda –tanzania) pamoja na ujenzi wa makao makuu ya nchi Dodoma.

Aidha aliongeza kuwa katika mkutano huo ambao unatarajiwa kuhudhuliwa na wakandarasi zaidi ya 200 ambao watatoa mawazo yao kuelekea ujenzi wauchumi wa viwanda kama sera ya awamu ya tano inavyoelekeza  ni muhimu kwa ujenzi wa taifa.

Mhandisi Mwakyambiki alisema kuwa katika kutambua mchango wa wakandarasi ni mara ya kwanza kwa mkutano huo kutokea Tanzania katika tasnia hiyo na mgeni rasmi katika mkutano huo atakuwa katibu mkuu wa sekta ya ujenzi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe Injinia Joseph Nyamuhanga.

Waziri Mwakyembe azindua Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ya kupata Uhuru

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amezindua Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ambayo yanalenga kuonyesha namna mashujaa wa Tanganyika walipambana kupata uhuru, maonyesho ambayo yatafanyika kwa muda wa mwezi mmoja katika Makumbusho ya Taifa- Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam. Uzinduzi wa maonyesho hayo ambao ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), kwa lengo ya kuendeleza juhudi za Uhifadhi wa Hifadhi ya Urithi Tanzania,hususani ya Ukombozi wa Afrika yanasimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa maonyesho hayo, Dkt. Mwakyembe alisema mradi huo wa kuhifadhi historia ya Ukombozi wa bara la Afrika ni muhimu kwa Tanzania kwani unaweza kusaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini kuliko ilivyo sasa kwani inawapa nafasi wageni ya kuona mambo tofauti na yaliyozoeleka pindi wanapokuja nchini. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ya kupata Uhuru. “Tuna mradi ambao utatupeleka mbali sana Watanzania, Afrika Kusini, Namibia, Angola hata wao wametuambia tusije shangaa sehemu hiyo ikawa inaleta watalii wengi zaidi kuliko wanaokuja kuangalia tembo na simba, urithi wa Afrika tumekabidhiwa na bara la Afrika ni wajibu wetu Watanzania kuusukuma huu mradi maana tumeshachelewa, Watanzania wengi labda hawaelewi mwaka 2011 kwa kushirikiana na UNESCO tulipeleka ombi AU la mradi huu wa bara la Afrika na wakaubariki huu mradi na wakaamua makao makuu yawe Tanzania na sisi tukachagua Dar na hapa kitajengwa kituo kikubwa kitakuwa na historia ya Ukombozi wa Afrika, sisi ndiyo viongozi wa huu mradi,” alisema Dkt. Mwakyembe. Alisema ili kufanikisha mradi huo tayari wameanza kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha pindi watakapojenga kituoambacho kitatumika kuhifadhi vitu mbalimbali ambavyo vilitumika katika kipindi cha ukombozi wa bara la Afrika kuwe na taarifa nyingi kuhusu bara la Afrika. “Tunawatumia wazee walio na historia ya ukombozi wa Afrika tumehoji zaidi ya wazee 100 na tunaendelea na hilo zoezi na tumebaini maeneo zaidi ya 200 Tanzania ambayo yanahitaji kuhifadhiwa, ni wajibu wangu kupeleka muswada bungeni ili tuyahifadhi na kuyalinda kwa kutumia sheria,” alisema Waziri Mwakyembe. Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini (EU), Roeland Van de Geer akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ya kupata Uhuru. Kwa upande wa Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini (EU), Roeland Van de Geer alisema ni muhimu kwa bara la Afrika kuwa na maonyesho ambayo yanaelezea historia ya bara hilo ili yatumike kuelezea kizazi cha sasa na kijacho namna nchi za Afrika zilipambana kupata uhuru na wao kama EU wataendelea kusaidia miradi mbalimbali yenye lengo ya kutunza urithi wa bara la Afrika. “Ni jambo la kujivunia kwa Umoja wa nchi za Ulaya kusaidia kufanikisha mradi huu … EU tumekuwa tukisaidia miradi mingi na hii yote ni kwa ajili ya kutunza utamaduni na urithi wa bara la Afrika, tumesaidia miradi mbalimbali nchini ikiwepo ya Olduvai na Ngorongoro na tutaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania kuendeleza maeneo ya kihistoria,” alisema. Afisa Mpango Kitaifa wa UNESCO, Nancy Kaizilege akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ya kupata Uhuru. Naye Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO kanda ya Afrika Mashariki na Afisa Mwakilishi wa Unesco Dar, Ann Therese Ndong- Jatta katika hotuba yake iliyosomwa na Afisa Mpango Kitaifa wa UNESCO, Nancy Kaizilege alisema ni jambo zuri kuwepo na makumbusho ambayo yanaeleza historia ya bara la Afrika na yatawza kuwapa nafasi watu mbalimbali kutoka mataifa ya nje ya bara la Afrika kuona na kujifunza historia ya Afrika. “Makumbusho haya ni muhimu kwasababu ni sehemu ya ukumbusho wetu kwa baadae, kupitia makumbusho haya tutaona historia ya bara la Afrika, historia ya mwanadamu na safari ya kutafuta uhuru ilivyokuwa,” alisema Kaizilege. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe na Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini (EU), Roeland Van de Geer wakikata utepe katika uzinduzi wa Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ya kupata Uhuru.Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa ameongozana na Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini (EU), Roeland Van de Geer na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuangalia vitu mbalimbali vya kihistoria ambavyo vimewekwa katikaMaonyesho ya Mashujaa na Mapambano ya kupata Uhuru.

RC GEITA KUWAPIMA MAOFISA UGANI UWEZO WA UTENDAJI KAZI ZAO ZA KILIMO

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, akimkabidhi mbegu bora ya mahindi, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel Lughumbi  wakati wa uzinduzi wa mashamba darasa ya mbegu za mahindi, mhogo na viazi lishe uliofanyika nje ya viwanja vya ofisi ya mkoa huo jana. Kushoto ni Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo   (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange.
 Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel Lughumbi akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kukabidhiwa mbegu hizo za mahindi zinazokabiliana na ukame  Wema.








 Ofisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, David Makabila akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Isamilo kabla ya uzinduzi wa shamba darasa la mbegu ya mahindi. Kutoka kushoto ni Mtafiti kutoka COSTECH, Dk.Beatrice Lyimo, Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula, Mtafiti Bestina Daniel na Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo   (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange.
 Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga Kilosa mkoani Morogoro,  Ismail Ngolinda, akitoa maelezo ya jinsi ya kupanda mbegu ya mahindi.
 wananchi wa Kijiji cha Isamilo wakiwa kwenye uzinduzi huo.
 Mkulima Hernick Elias wa Kijiji cha Isamilo akizungumzia changamoto za kilimo walizonazo
 Watafiti wakifanya vipimo kabla ya uzinduzi wa shamba la mbegu za mahindi katika kijiji cha Isamilo.
 Wakulima wa Kikundi cha Nguvumoja cha Kijiji cha Isamilo wakiwa shambani wakati wa uzinduzi huo.
 Mkulima wa Kijiji cha Isamilo, Salome Renatus akizungumza na waandishi wa habari.
  Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga Kilosa mkoani Morogoro,  Ismail Ngolinda, akionesha namna ya ujimbaji wa mashimo kabla ya upandaji wa mbegu za mahindi.
 Ofisa Ugani wa Kijiji cha Isamilo, Issa Pegeege, akionesha jinsi ya uwekaji mbolea kabla ya kupanda mbegu ya mahindi Wema.
 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari (kulia), kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, akiongoza wakulima kupanda mbegu ya mahindi kwenye shamba darasa katika Kijiji cha Isamilo.
 Mkulima wa Kijiji cha Kikundi cha Nguvu moja katika Kijiji cha Kamhanga, Hamisi King akitoa maelekezo wakati wa uzinduzi wa shamba darasa la mahindi katika kijiji hicho.
 Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga Kilosa mkoani Morogoro,  Ismail Ngolinda, akionesha namna ya ujimbaji wa mashimo kabla ya upandaji wa mbegu za mahindi katika Kijiji cha Isamilo. 
 Wakulima na wananchi wa Kikundi cha Kasimpya katika Kijiji cha Mnekezi kilichopo Kata ya Kaseme wakisubiri maelekezo namna ya kupanda mbegu za mahindi katika shamba darasa.
 Diwani wa Kata ya Kaseme, Andrew Kalamla akizungumza na wananchi katika uzinduzi wa shamba darasa hilo.
 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mnekezi.
 Mwakilishi wa Mkoa wa Geita, Emiri Kasagala, akihutubia katika uzinduzi huo kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo, Robert Gabriel
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, akipanda mbegu wakati wa uzinduzi wa shamba darasa katika Kijiji cha Mnekezi. Kulia ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa, Emiri Kasagala.

Na Dotto Mwaibale, Geita

MKUU wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel Lughumbi amesema ataanzisha utaratibu wa kuwapima maofisa ugani wa mkoa huo utendaji kazi wao ili kujua uwezo wa kila mmoja wao.

Hayo ameyasema  wakati Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ilipokuwa ikimkabidhi mbegu bora za mahindi, mihogo na viazi lishe ikiwa ni siku yake ya kwanza kufanya kazi katika mkoa huo tangu ateuliwe na Rais Dk.John Magufuli kushika wadhifa huo.

"Kilimo ni muhimu sana hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaingia katika uchumi wa kati wa viwanda hivyo nitaweka utaratibu wa kuwapima maofisa ugani wote wa mkoa huu ili niweze kujua utendaji kazi wao" alisema Lughumbi.

Lughumbi aliwataka maofisa ugani mkoani humo kuacha kukaa maofisi kwenye viyoyozi badala yake waende walipo wakulima kushirikiana nao kuwapa elimu ya kilimo ili kujikomboa kiuchumi kupitia kilimo.

Mkuu huyo wa mkoa ameahidi kununua viatu vya shambani 'gambuti' na koti na kuwa mara moja ataanza kutembelea wakulima katika maeneo yao ili kujua changamoto zao na kusema anapenda kuona mkoa wa Geita unakuwa namba moja kwa kilimo hapa nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH wakati wa kukabidhi mbegu hizo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari Msangi alisema kazi kubwa ya COSTECH ni kuishauri serikali katika masuala yote yanayohusu  Sayansi na Teknolojia na kusimamia tafiti zote za kisayansi katika maeneo mbalimbali na kilimo na kuhakikisha zinawafikia walengwa.

Alisema mbegu hizo walizozikabidhi zimefanyiwa utafiti na zitapandwa katika mashamba darasa na baadae kusambazwa kwa wakulima wengine ili kuondoa changamoto ya kukosekana kwa mbegu bora kutokana na wakulima kukabiliwa na mbegu ambazo zilikuwa na magonjwa kama batobato na ukame.

Akizungumzia mbegu bora ya viazi lishe alisema mbegu hiyo viazi vyake vinavitamini A ya kutosha ambayo ni muhimu kwa watoto na hiyo itawasaidia baadhi yao kuto kwenda Hospitali kuipata badala yake wataipata kwa kula viazi hivyo.

Msangi aliwaomba maofisa ugani pale wanapokuwa na changamoto mbalimbali za kazi yao wasisite kwenda COSTECH ili kusaidiana na kupeana mbinu mbalimbali za kilimo.

Mkulima wa Kijiji cha Isamilo, Hermick Elias alisema kukosekana kwa mbegu bora, wataalamu wa kilimo na kutofikiwa na pembejeo za kilimo kwa wakati ni moja ya sababu ambayo imewarudisha nyuma katika masuala ya kilimo lakini wanaamini kwa mbegu hizo walizoletewa na COSTECH itakuwa nu mkombozi kwao kwa kupata chakula na ziada watauza na kujipatia fedha za kuwasaidia.

Alisema kwa kilimo walichokuwa wakikifanya ekari moja walikuwa wakipata mahindi kuanzia magunia nane hadi tisa lakini kwa maelezo ya watafiti hao wa kilimo iwapo watatumia mbegu hiyo bora wataweza kupata magunia kuanzia 25 hadi 30.

Mkulima Salome Renatus aliipongeza serikali na COSTECH kwa kuwapelekea mbegu hizo hivyo wanatarajia kupata mazao yenye tija tofauti na awali.

Mbegu hizo zitapandwa katika mashamba darasa katika wilaya zote za mkoa wa Geita, Nyang'wale, Mbogwe,Chato na Bukombe.

MATUKIO KATIKA PICHA ZA KIKAO CHA KAMATI YA UTAWALA NA SERIKALI ZA MITAA MJINI DODOMA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala, Mheshimiwa George Mkuchika akisoma Taarifa ya Maboresho ya Mfumo wa Utumishi na Mshahara Serikalini (MCMIS) wakati Kamati hiyo ilipokutana na Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mjini Dodoma. Kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Laurean Ndumbaro.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa akifuatilia majadiliano ya Wajumbe wa Kamati yake wakati Kamati hiyo ilipokutana na Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala kwa ajili ya kupokea na kujadili Taarifa ya Maboresho ya Mfumo wa Utumishi na Mshahara Serikalini (MCMIS), Kulia kwake ni Katibu wa Kamati hiyo, Eunike Shirima.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakiwa katika kikao na Watendaji wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala ambapo leo walijadili Taarifa ya Maboresho ya Mfumo wa Utumishi na Mshahara Serikalini (MCMIS), Kulia kwake ni Katibu wa Kamati hiyo, Eunike Shirima.

Wafanyakazi 143 Wa Ofisi Ya Rais Utumishi Wahamia Dodoma Awamu Ya Pili

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bibi. Dorothy Aidan Mwaluko akiagana na Kiongozi wa msafara wa magari yaliyobeba mizigo ya ofisi hiyo ikiwa ni muendelezo wa zoezi la kuhamia Dodoma leo Jijini Dar es Salaam. Jumla ya wafanyakazi 143 wameagwa katika awamu hii ya pili, ambapo awamu ya kwanza waliondoka wafanyakazi 78. Katikati mwenye miwani Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bibi. Jane Kajiru.
Gari lililobeba nyaraka na vifaa vya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora likijiandaa kuondoka katika viwanja vya ofisi hiyo iliyopo Magogoni leo jijini Dar es Salaam. Jumla ya wafanyakazi 143 wameagwa katika awamu hii ya pili, ambapo awamu ya kwanza waliondoka wafanyakazi 78.
Baadhi ya wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakiwapungia mikono ya kwaheri madereva wa magari yaliyobeba mizigo ya ofisi hiyo ikiwa ni muendelezo wa zoezi la kuhamia Dodoma leo Jijini Dar es Salaam. Jumla ya wafanyakazi 143 wameagwa katika awamu hii ya pili, ambapo awamu ya kwanza waliondoka wafanyakazi 78.

Picha na: Frank Shija – MAELEZO

NAIBU WAZIRI LUGOLA AFANYA ZIARA ENEO LA TANDALE KWA MTOGOLE NA KUZINDUA OPERESHENI YA MIEZI MIWILI YA KUSAFISHA MITO NCHI NZIMA


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Kangi Lugola akizungumza na waandishi wa habari na wakazi wa eneo la Tande kwa Mtogole wakati wa ziara ya waziri huyo ya kuzindua operesheni ya miezi miwili ya kusafisha mito nchi nzima.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Kangi Lugola akikagua eneo la Mto Ng’ombe eneo la Tandale kwa Mtogole wakati wa ziara ya waziri huyo ya kuzindua operesheni ya miezi miwili ya kusafisha mito nchi nzima.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Kangi Lugola akisafisha eneo la Mto Ng’ombe kuashiria uzinduzi wa operesheni maalum ya miezi miwili ya kusafisha mito nchi nzima.
Eneo la Mto Ng’ombe likiwa limejaa taka ngumu kama zilivyokutwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Kangi Lugola wakati wa ziara ya waziri huyo ya kuzindua operesheni ya miezi miwili ya kusafisha mito nchi nzima.


Picha na Eliphace Marwa – Maelezo

Monday, October 30, 2017

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI, JAPHET HASUNGA ATEMBELEA MAPOROMOKO YA MTO KALAMBO AMBAYO NI YA PILI KWA UREFU BARANI AFRIKA

Na Hamza Temba - WMU

SERIKALI imesema imedhamiria kufungua utalii wa Kanda ya Kusini ili kupanua wigo wa vivutio vya utalii nchini na hatimaye kuongeza idadi ya watalii na kipato kwa Serikali na jamii kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga katika kijiji cha Kapozwa Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutembelea Maporomoko ya Mto Kalambo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya Maporomoko ya Tugela yaiyopo nchini Afrika ya Kusini.

Alisema kwa sasa vivutio vingi vinavyotumika kwa utalii nchini ni vile vya ukanda wa Kaskazini hususan vya wanyamapori ambavyo vimeanza kuelemewa kutokana na watalii wengi kutembelea ukanda huo zaidi kuliko Kanda ya Kusini ambayo pia ina vivutio mbalimbali vya asili.

Alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo benki ya Dunia kupitia mradi wa REGROW imepanga kuboresha miundombinu ya vivutio vya utalii vya Kanda ya Kusini na kuvitangaza ili kuimarisha sekta hiyo muhimu ambayo inachangia asilimia 25 ya mapato yote ya kigeni na asilimia 17.5 ya pato la taifa.

Katika ziara yake hiyo Mkoani Rukwa, alitembelea eneo la Hifadhi ya Msitu ya Mto Kalambo na kukagua ujenzi unaoendelea wa ngazi maalum zitakazowawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo ambacho ni mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. 

Alisema Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania inajenga ngazi hizo ili kuongeza thamani ya maporomoko hayo huku akiagiza Wakala hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine kuongeza juhudi za uwekezaji ili kuimarisha utalii wa kivutio hicho na kupanua kanda yote ya kusini.

"Tumekusudia kupanua wigo wa vivutio vyetu vya utalii kwa kufungua Kanda hii ya Kusini ambayo ina vivutio vingi ambavyo havijachangia ipasavyo kwenye uchumi wetu, maporomoko haya ni moja ya kivutio adimu katika ukanda huu. 

"Ni wakati muafaka sasa tushirikiane kuhamasisha wawekezaji kujenga mahoteli ya kisasa katika eneo hili, tuone uwezekano wa kuanzisha utalii wa 'cable cars' kuwezesha watalii kuona maporomoko kiurahisi, tujenge maeneo ya kupumzikia ili kuweka mazingira rafiki ya kupata watalii wengi na mapato yaongezeke" alisema Hasunga.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi wa kijiji cha Kapozwa ambao wanaishi jirani na hifadhi hiyo kushirikiana na Serikali katika uhifadhi wa uoto wa asili wa hifadhi hiyo pamoja na kudumisha tamaduni zao kwa kusajili vikundi vya ngoma na kutunga nyimbo za kabila lao kwa ajili ya kutumbuiza watalii watakaofika kuona maporomoko hayo na hivyo kujitengenezea kipato kupitia utalii wa Kiutamaduni.

Pamoja na Maporomoko hayo kivutio vingine kinachopatikana ukanda wa kusini ni Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo ni ya pili kwa ukubwa nchini baada ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti, hifadhi hii inasifika kwa kuwa na tembo wengi kuliko hifadhi nyingine nchini.

Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ni kivutio kingine katika ukanda huu ambacho sifa yake kubwa ni uwepo wa aina nyingi za maua ndwele ya asili ambayo hayapatikani kwingineko duniani, sifa hiyo imesababisha wenyeji kuita hifadhi hiyo 'Bustani ya Mungu'. Wataalamu wa uhifadhi wanasema endapo maua yaliyopo Kitulo yangekuwa ni wanyamapori basi hifadhi hiyo ingeizidi wanyama waliopo Serengeti.

Vivutio vingine ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Katavi ambayo ni ya tatu kwa ukubwa nchini, Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa, Mikumi, Mahale, Gombe, Pori la Akiba la Selous, Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Mlima Rugwe na Kimondo cha Mbozi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) akiteta jambo na Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni ya Greens Construction Limited, Hamimu Bakari wakati akishuka kwenye ngazi maalum zinazojengwa na mkandarasi huyo kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kushoto) akiteta jambo na Katibu Tawala Wilaya ya Kalambo Frank Schalwe wakati akishuka kwenye ngazi maalum zinazojengwa kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. 
Meneja wa TFS Wilaya ya Kalambo, Joseph Chezue (kushoto) akimuonyesha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) ngazi maalum zinazojengwa kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18.
 Muonekano wa ngazi hizo kuelekea kwenye Maporomoko ya Mto Kalambo.
Muonekano wa ngazi hizo.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (katikati) akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kukagua ujenzi wa ngazi maalum zinazojengwa kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura. 
Baadhi ya washiriki wa ziara hiyo wakishuka kwenye ngazi ambazo ujenzi wake bado unaendelea. Ujenzi huo ukikamilika ngazi hizo zitakuwa na urefu wa mita 227.
Ngazi hizo zimejengwa kwenye ukingo wa korongo la Mto Kalambo.
Sehemu ya juu ya Maporomoko ya Mto Kalambo.
 Muonekano wa mto Kalambo ambao unaotengeneza Maporomoko ya Mto Kalambo (Kalambo Falls)
Taswira ya maporomoko ya mto Kalambo kutokea angani (Picha hii ni kwa hisani ya Mtandao)

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...