Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Robert Paschal (Aliyevaa Koti waliosimama) akiongea na Wakuu wa Idara mbalimbali wa Halmashauri wa Wilaya ya Kilombero kuhusu Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania. Picha na Habari na Saidi Mkabakuli
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Bw. Lephy Gembe (Katikati) akizungumza na maafisa wa kutoka TADB wakati walipomtembelea Ofisini kwake. Wanaomsikiliza ni Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Robert Paschal (Wapili kushoto) na Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa TADB, Bw. Geofrey Mtawa (Kulia) na Afisa Maendeleo ya Biashara Mwandamizi wa TADB, Bw. George Nyamrunda (Kushoto).
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Bw. Lephy Gembe (Kulia) (Kushoto) akimsikiliza kwa makini Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Robert Paschal wakati walipomtembela Ofisini kwake.
Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Robert Paschal (Wapili kushoto) akiutambulisha msafara wa maafisa wa TADB waliomtembelea Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Bw. Lephy Gembe (Katikati). Wengine pichani ni Afisa Maendeleo ya Biashara Mwandamizi wa TADB, Bw. George Nyamrunda (Kushoto) na Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa TADB, Bw. Geofrey Mtawa (Kulia).
………………………………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu,
Benki mpya ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeaswa kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Bw. Lephy Gembe wakati akiongea na Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Robert Paschal alipomtembelea Ofisini kwake.
Bw. Gembe alisema kuwa ili kuinua uzalishaji wenye tija katika Sekta ya Kilimo kwa kuendeleza TADB ina wajibu wa kutoa elimu ya kina kuhusu kilimo cha kisasa kwa kutilia mkazo kuhusu miundombinu muhimu ya kilimo mathalani skimu za umwagiliaji za kilimo ili kuongezea tija shughuli hizo za kilimo.
“TADB muna wajibu wa kuhamasisha kilimo cha kisasa na cha kibiashara kwa wakulima wadogo wadogo ili waweze kubadilisha fikra zao kutoka kilimo cha mazoea na kufikiria kilimo cha kisasa chenye tija kitakachoongeza kipato cha wakulima hao,” alisema Bw. Gembe.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Kilombero aliongeza kuwa TADB inapaswa kutekeleza kwa vitendo juhudi za Serikali za kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania kupitia kilimo ambacho kwa mujibu wa takwimu kinaajiri zaidi ya asilimia 75 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini na pia kutoa kiasi cha zaidi ya asilimia 65 cha mali ghafi kwa ajili ya viwanda vya nchi.
Bw. Gembe alisema kuwa ili kufikia malengo yake TADB inapaswa kuwa na wataalamu wa utafiti na maendeleo ili waweze kuratibu taarifa za utafiti na maendeleo ya Kilimo, hali ya hewa, udongo unaofaa kwa Kilimo, pamoja na hatua nyingine za kuhuisha maendeleo kwenye Kilimo.
Akizungumza katika ziara hiyo Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Robert Paschal alisema kuwa TADB imejipanga kutoa mikopo ya kilimo katika makundi matatu ambayo ni Mikopo ya Muda Mfupi, Mikopo ya Muda wa Kati na Mikopo ya Muda Mrefu kwa kutumia njia mbalimbali.
Akizitaja njia ambazo TADB inatumia kutoa mikopo hiyo, zinajumuisha pamoja na mambo mengine, mikopo ya moja kwa moja kwa vikundi vya wakulima wadogo wadogo; kutoa mikopo kwa njia ya marejesho taasisi zinazokopesha; utoaji wa mikopo kwa pamoja na kushirikiana na taasisi/benki zingine; pamoja na mikopo ya miundombinu inayolenga kupunguza mapengo ya upatikanaji wa fedha katika minyororo ya ongezeko la thamani ya kipaumbele.
Bw. Paschal aliongeza kuwa kwa kuanzia, TADB imelenga uwekezaji katika maeneo nane (8) ya minyororo ya uongezaji wa thamani ambayo ni: nafaka, kilimo cha mbogamboga, kilimo cha bidhaa za viwanda, mbegu za mafuta, ufugaji wa ng’ombe, ufugaji kuku, ufugaji wa samaki na bidhaa za misitu.
Aliongeza kuwa Benki pia inajitahidi kusimamia fedha kutoka kwa wafadhili wengine ambazo zimeelekzwa kwenye kuendeleza kilimo.
Mkurugenzi huyo wa Mikopo alitumia fursa hiyo kumuomba ushirikiano Mhe. Gembe ili kuhakikisha mikopo hiyo inarudishwa kwa wakati.
“Ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, TADB inafanya kazi kwa karibu na washirika mbalimbali wa kimkakati pamoja wadau wengine muhimu kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo ukiwa ni mdau muhimu, tunakuomba ushirikiano katika kutimiza malengo ya kuanzishwa kwa TADB,” aliomba Bw. Paschal.
Kwa mujibu wa Bw. Paschal wadau wengine wa TADB ni pamoja na Serikali, Wizara na Wakala mbalimbali wa Serikali; Mashirika; Serikali za Mitaa, Sekta Binafsi, benki na taasisi za fedha, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Wafadhili wa ndani na wa Kimataifa, Taasisi za Utafiti na Umma kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment