- Ni tamthiliya inayohusu simulizi na visa vya kweli katika maisha ya watu.
- · Itaonekana katika chaneli ya StarTimes Swahili, mahususi kwa vipindi vinavyotumia lugha ya Kiswahili inayoonekana pia nchini Kenya.
- · StarTimes yahamasisha watanzania kuchangamkia fursa kwa kutengeneza filamu na tamthiliya ili ziweze kuonekana kupitia chaneli hiyo ili kupanua wigo wa mashabiki wao.
Katika kuboresha maudhui yanayotumia lugha ya Kiswahili, kampuni ya StarTimes Tanzania kupitia chaneli yake mahususi kwa vipindi vya Kiswahili ya StarTimes Swahili imewatangazia wateja wake ujio wa tamthiliya mpya na ya kusisimua ya ‘Scars au Makovu’ itakayoanza kurushwa siku ya Jumatatu ya mwezi Mei 2, 2016 saa 2:30 usiku.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa tamthiliya hiyo Meneja wa Vipindi na Maudhui wa StarTimes Tanzania, Bi. Paulina Kimweri amebainisha kuwa tamthiliya ya ‘Scars’ itakuwa ni ya aina yake na kusisimua zaidi kwani inagusa zaidi maisha halisi ya kila siku.
“Tamthiliya hii ni tofauti na zingine kwani ndani yake ina visa na simulizi za kweli kabisa za maisha ya wahusika waliocheza ndani yake. Masuala kama ya changamoto mbalimbali wanazopitia watu kwenye familia zao kama vile mateso, udhalilishaji na unyanyasaji wanaopitia wanawake katika ndoa zao. Haya yote yatakuwa yakisimuliwa na kuonekana kwa wateja na watazamaji wa chaneli ya StarTimes Swahili.” Alielezea Bi. Kimweri
Meneja huyo wa Maudhui katika kampuni hiyo inayotoa huduma ya matangazo ya luninga kwa njia ya dijitali alifafanua zaidi kuwa, “Lengo kubwa la kuanzishwa na kuwepo kwa chaneli hii mahususi kwa vipindi vya Kiswahili si tu kuwaburudisha wateja wetu kwa maudhui mazuri bila pia kukuza lugha ya Kiswahili kwani chaneli hii inaonekana katika nchi za Tanzania na Kenya. Pia hutoa fursa kwa watayarishaji na wasanii wa vipindi vya Kiswahili baina ya nchi hizi. Hivyo basi hii ni fursa kubwa ya kufurahia wasanii wetu na kuipaisha lugha yetu ya Kiswahili ambayo kwa sasa inazidi kupaa katika anga za kimataifa.”
“Nina imani kubwa na tamthiliya hii ya ‘Scars’ kwamba itapendwa sana na wateja wetu kwani inagusa maisha halisi kwa simulizi zitakazopatikana ndani yake. Katika uchaguzi wa tamthiliya tunazotaka zionekane kwa wateja wetu huwa tunazingatia sana suala la ujumbe na mafunzo yanayopatikana ndani yake na si burudani pekee. Hivyo, basi ningependa kuchukua fursa hii kuwataka wateja wetu na watanzania wapenda tamthiliya tamthiliya kukaa mkao wa kula na kutega macho ya mbele ya luninga zao ifikapo siku ya Jumatatu na zinginezo kila ifikapo saa 2:30 usiku kwenye chaneli ya StarTimes Swahili. Nawaomba walipie kwani malipo yetu ni nafuu ili kila mtu aweze kufurahia huduma zetu.” Alihitimisha Bi. Kimweri
Mbali na tamthiliya mpya ya ‘Scars au Makovu’ pia kupitia chaneli ya StarTimes Swahili ambayo inaonekana kwenye kisimbuzi cha kampuni ya Startimes kwa nchi za Kenya na Tanzania pia kuna tamthiliya moto moto zinazoonekana kwa sasa kama vile; Urembo, Fihi, Majaribu, Kijakazi, Majaribu, Kivuli na Sumu la Penzi.
Chaneli hii imeanzishwa mahususi kabisa katika kuonyesha vipindi vyenye maudhui ya lugha ya Kiswahili ambapo lugha hiyo inazungumzwa katika nchi nyingi za Afrika ya Mashariki na Kati. Kupitia chaneli hii si tu kukuza lugha ya Kiswahili bali pia ni fursa kubwa kwa wasanii kuonekana na kujitangaza kupitia kazi zao ili ziweze kuonekana katika soko la Afrika ya Mashariki. Hivyo basi hii fursa kubwa kwa wasanii wa nchini Tanzania kuchangamkia faida zinazokuja na matangazo ya dijitali kwa kupeleka kazi zao katika kampuni ya StarTimes ili ziweze kuonekana hewani.
No comments:
Post a Comment