Monday, February 17, 2014

Tumekubaliana Kuacha Unyonge! Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete Awaambia Wajumbe Wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM

  Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongoza kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) katika jengo la White House mjini Dodoma jana, akiwa meza kuu na Makamu wa Rais wa CCM visiwani na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein, na Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana. 
 
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amewataka wanachama wake kuacha unyonge na kujibu mapigo ya wapinzani hasa wale ambao wanaendesha siasa za vurugu katika kampeni za chaguzi mbalimbali nchini.
 
Rais Kikwete amesema kuwa uvumilivu una ukomo, na kwamba sasa wanachama wa CCM hawana budi kuacha unyonge, kutokana na siasa hizo za vurugu zinazoendeshwa na vyama vya upinzani.
 
Aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akifungua kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kitakachokutana kwa siku mbili chini ya uenyekiti wake, ambacho ajenda kuu ni kuzungumzia Bunge Maalumu la Katiba.
“Tumelizungumzia hili katika Kamati Kuu, tumekubaliana kuacha unyonge (makofi). Ndiyo watu wamelisema hili katika Kamati Kuu, tumesema jamani tumekubaliana kuacha unyonge,”
“Wacha wakaseme (waandishi wa habari), ndio tumekubaliana kuacha unyonge. Kabisa. Hata kama leo katika taarifa za habari, zisiwekwe habari nyingine, msikike ninyi tu. Uvumilivu una ukomo wake.”
alisema Rais Kikwete ambaye wakati anafungua kikao hicho waandishi wa habari walikuwamo.Mwenyekiti huyo wa CCM alisema wamefikia hatua hiyo kwa sababu yanayotokea yanasikitisha sana na akatoa mfano wa matukio kadhaa ya uvunjifu wa amani katika kampeni katika maeneo ya Igunga mkoani Tabora na Kahama mkoani Shinyanga.
“Maana tunashindana na wenzetu wagomvi maana wao ugomvi ndio sehemu ya mwongozo wa kufanya kazi ya siasa. Maana pale Kahama kijana wamemtoa macho kwa bisibisi. Acheni unyonge (makofi).
 
“Nasema kwa kweli kwa sababu yanayotokea yanasikitisha. Pale Igunga kijana yule wamemmwagia tindikali, pale Kahama kijana wamemtoa macho kwa bisibisi. Tuache unyonge,”
alisisitiza Rais Kikwete huku akishinikizwa kwa shangwe za CCM Oyee, Mapinduzi Daima.
 
Ingawa Rais Kikwete hakutaja chama, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekuwa kikihusishwa na vurugu za uchaguzi katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya Igunga na Kahama katika uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika hivi karibuni na pia katika chaguzi ndogo za ubunge.
 
Akizungumzia uchaguzi mdogo wa kata 27 zilizofanyika hivi karibuni na CCM kuzoa kata 23, Rais Kikwete aliwapongeza wanaCCM kwa ushindi huo, lakini akawapa changamoto ya kuhakikisha wanarejesha kata hizo nne zilizokwenda kwa vyama vya upinzani.
“Huu ni ushindi mkubwa sana, ushindi mnono. Ni vizuri kutumia nafasi hii kujipongeza na kuwapongeza wenzetu kwa kazi nzuri, kazi nzuri waliyoifanya ya kujenga chama,”
 
“Lakini tukumbushane kwamba kata nne hatukuzipata, hivyo tuna kazi ya kuzikomboa, sisi wakati wote nia yetu ni kushinda, kushindwa haiwezekani.”
alisema Mwenyekiti huyo wa CCM na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
 
Aidha, alizungumzia uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, akisema hadi sasa hali ni shwari, hakuna migawanyiko wala misukosuko kama ilivyokuwa kwa Jimbo la Arumeru Mashariki ambalo alisema tangu mwanzo hadi mwisho, hali haikuwa shwari.
 
Alisema hadi sasa wana uhakika wa ushindi katika jimbo hilo, lakini akawataka wanaCCM kujiandaa vyema kwa kila hali na kuhakikisha ushindi unapatikana katika jimbo lililoachwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa. Mwanawe Geoffrey ndiye mgombea wa CCM.
 
Pia aliwataka wanachama na viongozi wa Jimbo la Chalinze mkoani Pwani, nao kujiandaa kwa uchaguzi mdogo kwa sababu tayari Spika wa Bunge, ametoa taarifa serikalini kuhusu kuwa wazi kwa jimbo hilo kutokana na kifo cha mbunge wake, Said Bwanamdogo.
“Msikae tu kusubiri na kuendelea kuomboleza, kwa sababu Serikali haiombolezi, wao wanachotaka ni uchaguzi ujazwe, shughuli ziendelee. Maana watu wanaweza kusema hata orobaini bado. Kule Arumeru tuliambiwa tumbo bado halijapasuka. Kwani kwa Mgimwa orobaini tayari, mbona mchakato umeanza.
 
“Ninyi fanyeni mchakato, orobaini yetu mnaweza kufanya wakati mambo mengine yakiendelea. Tujiandae mapema ili kuhakikisha tunashinda,”
alisema Mwenyekiti huyo wa CCM na kuwapongeza viongozi wa mkoa na wilaya waliofanikisha ushindi katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki ambako mgombea wao, Mahmoud Thabit Kombo alishinda.

Alisema CCM ilibidi kumtosa aliyekuwa mbunge wao, Mansour Yussuf Himid, kwa sababu alikuwa akivaa magwanda ya chama hicho, lakini alikuwa akipinga sera na taratibu za chama hicho tawala.
“Kila akifungua mdomo wake anaitukana CCM, kila akifungua mdomo anapingana na sera za CCM. Tukasema inatosha, bora kuwa na mpinzani huko nje kuliko huyu, ndio maana niliwahi kusema katika NEC moja hapa kuwa sijui mtu anasema nitahama CCM, nikasema nendeni sasa hivi,”alisema Kikwete.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...