Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe, Dar es salaam
Tel: 0712461976 au 0764302956
“Hawa vijana ni kama mahindi machanga yanayochipukia, wasikatishwe tamaa hata kidogo. Kile walichopata dhidi ya Msumbiji sio mafanikio hata kidogo, ndio kwanza wanajengwa kwa mafanikio ya baadaye. Nawaomba Watanzania waisapoti timu hii kwani itakuja kufanya kazi nzuri”. Ni maneno aliyetamka Kocha wa Tanzanite Rogasian Kaijage kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Afrika kusini.
Hatimaye alichokuwa anasema kilitimia jana uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam, baada ya kikosi cha timu ya Taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20, maarufu kwa jina la Tanzanite kukubali kulala kwa mabao 4-1 dhidi ya Afrika kusini `Basetsana` kwenye mchezo wa raundi ya pili ya mchujo ya kufuzu kombe la Dunia mwakani nchini Canada.
Amogelang Motay alikuwa mchezaji wa kwanza wa Afrika kusini kutikisa nyavu za Tanzanite kufuatia kuwazidi ujanja vijana wa Tanzanite waliowatoa Msumbiji raundi ya kwanza kwa mabao 15-1.
Baada ya kufungwa bao hilo, Tanzanite walipiga hesabu nzuri na kusawazisha dakika ya 13 kupitia kwa nyota wake Theresa Yohana aliyepiga shuti umbali wa mita 30 na kutingisha nyavu za Afrika kusini.
Kama unajua, unajua tu!, mnamo dakika ya 17, Afrika kusini waliandika bao la pili kupitia kwa Shiwe Nogwanya na lilidumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili Afrika Kusini waliendelea kulisakama lango la Tanzanite na dakika ya 61, walitumbukiza gozi kimiani kupitia kwa Mosili Makhoali na kufanya ubao wa Matangazo wa uwanja wa Taifa kusomeka 3-1.
Wimbo ukiimbwa: Hakika ilikuwa huzuni sana uwanja wa Taifa kufuatia kuimbwa kwa wimbo wa kuomboleza kifo cha kiongozi wa zamani wa Afrika kusini, Nelson Mandela aliyefarika dunia.
Afrika kusini walionesha ukomavu mkubwa na uzoefu wao ,dakika ya 78 walikamilisha idadi ya mabao 4-1 baada ya kufunga kupitia kwa Mosil Makhoali.
Matokeo hayo ni mabaya kwa Tanzanite, kwani wanatakiwa kufanya kazi kubwa ya kufunga mabao 5-0 huko Afrika kusini endapo watahitaji kusonga mbele.
Kwa uwezo wa vijana wa Afrika kusini, umakini wao, uzoefu wao inaonekana safari ya Tanzanite ndio imeishia hapo, ingawa katika mpira wa miguu chochote kinaweza kutokea.
Kama Afrika kusini wameweza kufunga mabao 4-1 ugenini, kwanini Tanzanite wasifunge matano Ugenini, inawezekana katika matokeo ya mpira wa Miguu.
Afrika kusini waliingia katika mchezo wa jana wakiwa na majonzi ya kufiwa na Rais wao wa kwanza, Mzee Tata Nelson Madiba Mandela, lakini walionekana kutotaka kushindwa hata kama wapo wakati mgumu wa majonzi.
Uwanjani uliimbwa wimbo maalumu wa Maomboleza wa kumkumbuka Tata Madiba Mandela, Kiongozi mweusi aliyetukuka kwa kupinga ubaguzi wa rangi.
Matokeo sio `Ishu` sana kwa Tanzanite, na ndio maana kocha Kaijage alisema vijana wake ndio kwanza wameanza safari ya kutafuta mafanikio.
“Vijana hawa wanahitaji kupewa moyo. Najua wazi, Wanzania wengi tunahitaji mafanikio ya haraka, kwa hili naombeni mnielewe vizuri kuwa, Tanzanite ni kama mahindi machanga yanayochipukia, yanahitaji kupaliliwa,kuwekewa mbolea ili yazidi kukua na kuzaa. Lazima waungwe mkono jamani!”. Alisema Kocha Kaijage.
Kaijage alikiri wazi kuwa mchezo ungekuwa mgumu sana kutokana na Afrika kusini kuwa na kiwango cha juu zaidi.
“Wengi waliamini kuwa wenzetu wapo katika majonzi na ingeathiri mchezo. Binafsi nilikuwa najua kuwa watashindana sana kutafuta matokeo mazuri. Tumezidiwa na kufungwa bao nyingi nyumbani, Lakini watu wa mpira wanajua kuwa mambo kama haya yanatokea”. Alisema Kaijage.
Awali wakiwa kambini Ruvu mkoani Pwani, Tanzanite walichanganywa na dada zao wa Twiga Stars ili kuwapa uzoefu, zoezi hilo linaonesha matunda kwani vijana wanaendelea kuimarika na kuwa na moyo wa kukubali kazi yao na kushindana.
Mtifuano!: Vijana wa Tanzanite walipambana sana, lakini uwezo mkubwa wa Afrika kusini uliwabeba na kupata matokeo ya 4-1. (Picha kwa hisani ya Blog ya Lenzi ya Michezo)
Pia mgeni rasmi katika mchezo wa jana, waziri wa habari, vijana, utamaduni na michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara aliwataka vijana wa Tanzanite kutokufa moyo kwani mpambanaji kamwe hakati tamaa.
Mukangara aliwaomba vijana kusahau matokeo hayo na kwenda kukaa chini kujipanga kwa mechi ya marudiano, huku akiliomba benchi la ufundi chini ya kocha mkuu Rogasian Kaijage kuhakikisha linaweka mikakati ya kushinda ugenini na kusonga mbele.
Wakati Tanzanite wakileta machungu kwa Watanzania, kaka zao wa Kilimanjaro Stars jana waliwapa raha na burudani kubwa mashabiki wa soka baada ya kuwatoa mabingwa watetezi wa kombe la Mataifa ya Afrika mashariki na kati, CECAFA Challenge, Uganda The Cranes, kwenye mchezo wa robo fainali ya kwanza ya michuano hiyo, uwanja wa Manispaa Mombasa.
Stars walishinda kwa penati 3-2 baada ya dakika tisini kumalizika kwa sare ya 2-2.
Sasa Kili Stars inajiandaa na mchezo wa nusu fainali Desemba 10 mwaka huu dhidi ya wenyeji wa michuano hiyo, Timu ya Taifa ya Kenya, Harambee stars.
No comments:
Post a Comment