TIMU ya Taifa ya Tanzania bara, The Kilimanjaro Stars imefanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya kombe la Mataifa ya Afrika mashariki na kati, CECAFA Challenge 2013 baada ya kuwafunga waliokuwa mabingwa watetezi, na wababe wake mfululizo kwa mechi za hivi karibuni , Uganda The Cranes kwa mikwaju ya penati 3-2 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya ngwe ya dakika 90 kwenye uwanja wa Manispaa, Mombasa.
Katika mchezo huo, Uganda walikuwa wa kwanza kuandika bao la kuongoza dakika ya 16 kupitia kwa mshambuliaji wake anayekipiga klabu ya Gor Mahia ya Kenya , Dani Sserunkuma , baada ya kupokea krosi ya Khamis Friday Kiiza aliyemtoka beki wa Stars, Erasto Nyoni na kuachia shuti la chini lililompita kipa mkongwe anayecheza Gor Mahia pia, Ivo Philip Mapunda.
Mrisho Khalfan Ngassa `Anko` aliisawazishia Kili stars bao hilo dakika mbili baadaye kufuatia kuwazidi ujanja mabeki wa Uganda, akimalizia mpira murua uliochongwa na jembe la TP Mazembe, Mwana Ally Samatta.
Pia Samatta aliangushwa nje kidogo ya eneo la hatari na Ngassa kwa mara nyingine alipewa majukumu ya kupiga mpira na bila kufanya makosa aliachia shuti lililotinga moja kwa moja nyavuni.
Hadi mapumziko, Kili stars walikuwa mbele kwa mabao 2-1, huku kipinidi cha pili kikisubiriwa kwa hamu kuona nani ataibuka na ushindi.
Wamefuta uteja: Leo hii Kilimanjaro Stars wameondoa unyonge baada ya kuwashinda Waganda kwa penati 3-2 na kutinga hatua ya nusua fainali ya CECAFA 2013
Kipindi cha pili kilipoanza, majanga yaliikumba Stars baada ya kiungo wake mahiri, Salum Abubakar `Sure Boy` kuoneshwa kadi nyekundu baada ya kumfanyia madhambi Sserunkuma.
Dakika ya 73, mabeki wa Stars walifanya makosa na kumruhusu Martin Mpuga kusawazisha bao hilo akiunganisha mpira wa kona uliochongwa na Godfrey Walusimbi.
Dakika 90 zilimalizika kwa sare ya 2-2 na ndipo sheria ya mikwaju ya penati ilipotumika.
Kipa Ivo Mapunda alikuwa shujaa baada ya kuokoa mikwaju miwili ya penalty ya Dani Sserunkuma na Khalid Aucho wa Uganda .
Mbali na kuokoa penalti hizo mbili, Uganda walipoteza penalti nyingine moja baada ya Godfrey Walusimbi kupiga na kukosa.
Khamis Kiiza na Emannuel Okwi ndiyo wachezaji pekee walioifungia Cranes penati katika mchezo wa leo ambao Uganda waliingia kwa ujasiri wa kuibuka na ushindi kufuatia kuwa na rekodi nzuri dhidi ya Stars.
Penati za Stars zilifungwa na nahodha Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’na Erasto Nyoni, wakati Mbwana Samatta na Amri Kiemba walikosa.
Hata hivyo, mshambuliaji wa Stars anayekupiga TP Mazembe ya DRC Kongo, Mbwana Ally Samatta ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa Robo Fainali hiyo ya Kwanza ya CECAFA Challenge.
Samatta amepewa tuzo hiyo inayoambatana na zawadi ya king’amuzi na kifurushi cha GOtv kufuatia kuwa chanzo cha mabao yote mawili ya Stars yaliyofungwa na Mrisho Khalfan Ngassa.
Aidha Samatta amepewa tuzo hiyo na kuwa mchezaji wa pili wa Kili Stars kuibuka kidedea katika tuzo hiyo kwani katika mchezo wa kwanza wa Stars hatua ya makundi dhidi ya Zambia uliomalizika kwa sare ya 1-1, kiungo Salum Abubakar `Sure Boy` aliteuliwa kuwa mchezaji bora.
Jembe la TP Mazembe: Mbwana Samatta ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa robo fainali ya kwanza ya CECAFA leo hii
Kwa matokeo ya leo, Kili stars wanarudia kuingia nusu fainali kama mwaka jana nchini Uganda, wakati The Cranes wamelitema kombe lao na kuliacha Mombasa Kenya na kurejea kufanya yao Kampala.
Fainali nyingine imepigwa jioni ambapo wenyeji Kenya wameshuka dimbani kukabiliana na Rwanda na kushuhudia Harambee stars wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 na kuwafungashia virago Amavubi.
Bao pekee la beki wa Azam FC ya Dar es Salaam, Joackins Atudo kwa penalti dakika ya 56 limewapeleka Kenya mbele ya safari ya kuusaka Ubingwa wa CECAFA katika ardhi yao 2013.
Kwa matokeo hayo Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars itamenyana na wenyeji, Harambee Stars katika Nusu Fainali ya Kwanza ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Desemba 10, mwaka huu Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Kenya.
Hongera Kilimanjaro Stars kwa kuwaondolea maumivu Watanzania ambao kwa muda mrefu sasa wamekuwa wanyonge kwa Waganda kila wanapokutana katika michuano mikubwa.
Safari bado ni ngumu, lazima vijana wakaze mwanzo mwisho kuhakikisha wanatwaa kombe hilo kama walivyofanya kwa mara ya mwisho mwaka 2010 chini ya Kocha Mdenmark, Jan Poulsen Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment