Friday, December 13, 2013

Rais Jakaya Kikwete Awajulia Hali Waziri wa Fedha William Mgimwa na Ofisa Mwandamizi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jenerali Vicent Kariongo Mritaba Afrika ya Kusini

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA 
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtembelea Waziri wa Fedha, Mheshimiwa William Mgimwa katika Hospitali ya Kloof mjini Pretoria, Afrika Kusini, ambako Waziri huyo amelazwa akitibiwa.

Rais Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini Afrika Kusini alimtembelea Waziri Mgimwa jioni ya  Jumanne, Desemba 10, 2013, baada ya kumaliza shughuli za jana za Kumbukumbu ya Kifo cha aliyekuwa kiongozi mashuhuri wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela.

Katika mazungumzo yaliyochukua kiasi cha robo saa, Waziri Mgimwa alimwambia Rais Kikwete: “Hali yangu inaendelea vizuri Mheshimiwa Rais na nakushukuru sana kwa kupata muda wa kuja kuniona. Inatia moyo na nguvu sana Mheshimiwa Rais.”

Naye Rais Kikwete amemtakia heri Waziri Mgimwa ambaye amekuwa kwenye hospitali hiyo kwa muda sasa na baadaye alipata nafasi ya kusalimia na wana-familia wa Mheshimiwa Mgimwa ikiwa ni pamoja na mke wake na binti yake mkubwa.

Wakati huo huo, Rais Kikwete juzi, Jumatano, Desemba 11, 2013, alimtembelea Ofisa Mwandamizi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jenerali Vicent Kariongo Mritaba ambaye amelazwa kwenye Hospitali ya Mifupa ya Lynnmed Clinic iliyoko eneo la Lynnwood mjini Pretoria.

Rais Kikwete amemtembelea Jenerali Mritaba akiwa njiani kwenda Uwanja wa Ndege wa Kituo cha Jeshi la Anga la  Waterkloof ili aweze kupanda ndege kurejea nyumbani.

Kabla ya kuondoka nchini, Rais Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi 91 wa wakuu wa Serikali na nchi waliotoa heshima za mwisho kwa mwili wa Mzee Mandela na kutia saini Kitabu cha Kumbukumbu cha Kifo cha kiongozi huyo ambaye hujulikana kwa jina maarufu la Madiba.

Viongozi hao walikuwa wa kwanza kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili huo ambao utalazwa kwenye Ofisi ya Urais wa Afrika Kusini zilizoko katika majengo ya Union Buildings, Pretoria.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
11 Desemba, 2013

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...