Tuesday, November 05, 2013

BALOZI SEFU IDDI AZIASA REDIO ZA JAMII KUWA CHACHU YA MAENDELEO VISIWANI ZANZIBAR

IMG_2183
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikata utepe kuzindua rasmi Redio Jamii ya Wilaya ndogo ya Tumbatu visiwani Zanzibar. Kushoto ni Kaimu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa (Unesco)Bw. Abdul Wahab Coulibaly wanaofadhili unzishwaji wa redio za jamii Tanzania Bara na Visiwani.
116
Mkurugenzi wa Kituo cha Redio Jamii cha Tumbatu Ali Khamis Mtwana akimpatia maelezo juu ya utendaji wa Kituo hicho Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kukizindua rasmi.
Kulia kwa Balozi Seif ni Kaimu Mwakilishi Mkazi wa Unesco Bw. Abdul Wahab Coulibaly na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbaouk.
123
Mkurugenzi wa Kituo cha Redio Jamii cha Tumbatu Ali Khamis Mtwana akifanya vitu vyake wakati akiwa hewani kurusha matangazo ya kituo cha Redio Jamii Tumbatu mara baada ya kuzinduliwa na Balozi Seif Ali Iddi. Kushoto kwa Balozi Sefu ni Kaimu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa (Unesco)Bw. Abdul Wahab Coulibaly wafadhili wa mradi huo.
IMG_2245
Meza kuu kutoka kushoto ni Kaimu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa (Unesco)Bw. Abdul Wahab Coulibaly, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Sefu Ali Iddi, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Pembe Juma Khamis, Waziri wa Habari Utamaduni Michezo na Utalii Mheshimiwa Said Ali Mbarouk, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Issa Mlingoti pamoja na Afisa Mipango Taifa wa Kitengo cha Mawasiliano na Habari na mratibu wa miradi ya UNESCO Yusuph Al-Amin.
IMG_2464
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu katika hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Matangazo ya Redio Jamii Kisiwani humo.
Na. Othman Khamis Ame
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Vituo vya Redio Jamii hapa Nchini vinapaswa kuwa chem Chem ya elimu itakayotoa manufaa kwa Jamii inayovizunguuka Vituo hivyo badala ya utaratibu wa kurusha vipindi vya muziki wakati wote.
Kauli hiyo aliitoa wakati akiizindua Redio Jamii ya Wilaya ndogo ya Tumbatu hapo katika jengo la Wilaya hiyo liliopo katika Kijiji cha Kichangani ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Balozi Seif alisema mijadala na nakala zinazohusiana na masuala ya Uchumi, siasa, jamii na Maendeleo ndio lengo lililokusudiwa katika uanzishwaji wa Redio hizo na kupelekea kuungwa mkono na Taasisi na mashirika ya maendeleo Duniani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka watendaji wa Redio Jamii Tumbatu kujitahidi kuwaelimisha wananchi kuhusu uvuvi bora na mambo mengi yanayohusiana na bahari kwani maisha ya wananchi hao yametegemea zaidi sekta ya bahari.
IMG_2262
Wakazi wa Tumbatu wakimsikiliza Makamu wa Rais wa Pili Balozi Sefu Ali Iddi wakati akisoma hotuba yake kwenye sherehe ya uzinduzi wa Redio Jamii ya Tumbatu.
IMG_2375
Kaimu Mwakilishi Mkazi Mwakilishi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa (Unesco)Bw. Abdul Wahab Coulibaly akitoa salamu zake katika hafla ya ufunguzi wa kituo cha redio jamii Tumbatu kilichopata msaada na ufadhili mkubwa kutoka shirika hilo.
Bw. Coulibaly amesema Redio waliyoikabidhi ni ya tatu kwa Zanzibar baada ya zile za Micheweni na Makunduchi huko kusini Unguja.
“ Tunategemea redio yenu ya jamii hapa Tumbatu itajikita zaidi katika kuwaelimisha wananchi wa Kisiwa hichi na maeneo ya jirani kuhusu athari za uvuvi haramu ambao unapigwa vita na Serikali kisheria “. Alisisitiza Balozi Seif.
Alitahadharisha jamii kwamba vyombo vya habari vina nguvu kubwa ambayo kama itatumika vibaya inaweza kuleta mifarakano mikubwa katika jamii na hivyo basi usalama na amani unaweza kuhatarishwa.
Balozi Seif alifahamisha kuwa chokochoko na fitna za kisiasa zikiachiwa na kuelekezwa katika vituo vya redio Jamii ni mwanzo wa kuathirika kwa vituo hivyo, watendaji pamoja na wananchi wenyewe.
“ Nia ya Redio jamii ni kuelimisha jamii na sio kupotosha. Hivyo Wanahabari wa Redio hizi wanapaswa kufanya utafiti wa kina wa Habari zao kabla ya kuzitoa, vyenginevyo zinaweza kupotosha jamii “. Alifafanua Balozi Seif.
Alileza kwamba lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuona vyombo vya Habari na utangazaji nchini vinasaidia kudumisha na kuimarisha usalama na amani hatimae kupata maendeleo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka watendaji wa Redio hiyo redio nafasi kwa wananchi wa rika, jinsia na kila makundi yote yanayostahiki kusikika katika jamii inayowazunguuka.
IMG_2403
Waziri wa Habari Utamaduni Michezo na Utalii Mheshimiwa Said Ali Mbarouk akisoma risala yake kwa wakazi wa Tumbatu kwenye sherehe za ufunguzi wa redio jamii kisiwani humo.
Balozi Seif alilishukuru Shirika la Elimu, Sayansi na Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa {UNESCO } kwa msaada wake mkubwa wa vifaa vya studio na mitambo ya kurushia matangazo kwa Redio Jamii ya Tumbatu.
Aliiomba taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa kuendelea kusaidia harakati nyengine za kijamii kila hali inaporuhusu na kitendo cha Uongozi wa Jumuiya hiyo kuahidi kukamilisha changamoto zinazokikabili kituo hicho ndani ya mwezi mmoja ujao ni cha kupigiwa mfano.
Akisoma Risala ya Wananchi wa Kisiwa hicho Afisa Tawala wa Wilaya Ndogo ya Tumbatu ambae pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Redio hiyo Ndg. Mohd Omar Hamad alisema uongozi wa Redio hiyo umekusudia kutoa vipindi vitakavyotumiwa na wanafunzi wa Maskuli na Madrasa za eneo hilo.
IMG_2336
Afisa Tawala wa Wilaya Ndogo ya Tumbatu ambae pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Redio hiyo Ndg. Mohd Omar Hamad akisoma taarifa yake mbele ya mgeni rasmi.
Ndg. Mohd alisema utaratibu huo ambao ni miongoni mwa mpango kazi wa Redio hiyo utasaidia wanafunzi hao kujiimarisha zaidi kielimu kwa kujijengea uwezo mkubwa wakati wanapokabiliana na mitihani yao.
Hata hivyo Afisa Tawala huyo wa Wilaya ndogo ya Tumbatu alielezea changamoto zinazokikabili kituo hicho cha Redio jamii Tumbatu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa jengo la kudumu ambapo hivi sasa wanatumia jengo la Ofisi ya Wilaya hiyo.
Akitoa Salamu za Shirika la Elimu, Sayansi na Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa { UNESCO } Kaimu Mwakilishi Mkazi wa Shirika hilo Bw. Abdul Wahab Coulibaly alisema Taasisi yake itaendelea kushirikiana na washirika wengine wa maendeleo katika kuunga mkono Vituo vya Redio Jamii.
Bw. Abdul Wahab Coulibaly alisema Redio Jamii Tumbatu iliyopata ufadhili wa Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la Unesco ina uwezo wa nguvu za Walti 300 ambazo zinaweza kuhudumia wasikilishaji zaidi ya Laki 150,000.
Akimkaribisha mgeni rasmi Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk alisema Redio Jamii Nchini tayari zimeshaonyesha mafanikio makubwa kwa kuisaidia kubadilisha mazingira ya Jamii kupitia taaluma inayotolewa kwenye vipindi vya Vituo hivyo.
Waziri Mbarouk alifahamisha kwamba Zanzibar hivi sasa ina vituo ishirini vya matangazo ya redio ikilinganishwa na kituo kimoja tuu cha Redio cha Serikali { STZ } kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
IMG_2339
Wanatumbatu wakitoa burudani ya Kaswida wakati wa sherehe za uzinduzi wa redio ya Jamii Tumbatu.
Alieleza kwamba kadri hali ya maisha inavyobadilika ndivyo sekta ya Habari inavyopanuka ikitoa fursa pia kwa redio nyengine za Jamii zilizoanzishwa katika Wilaya ya Micheweni Pemba na Mtengani Makunduchi Kusini Unguja kwa msaada mkubwa wa UNESCO kupiga hatua kubwa kimaendeleo.
Redio Jamii ya Kisiwa cha Tumbatu inayotumia masafa ya 94.99 F.M inasikika katika umbali wa Kilomita zaidi ya 15 unaokizunguuka kituo hicho. Hata hivyo Redio hiyo pia inawqeza kusikika hata katika eneo la Mji wa Zanzibar kutegemea hali ya hewa iliyopo.
IMG_2344
Wakazi wa Tumbatu wakicheza Kaswida kwa furaha bila kujali Mvua kali iliyokuwa inanyesha kisiwani hapo.
IMG_2387
IMG_2305
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Michezo na Utalii visiwani Zanzibar Mh. Hindi Hamadi akiwatunza mabinti waliokua wakitoa burudani ya kughani mashairi wakati wa sherehe hizo.
IMG_2251
Sehemu ya wakazi wa wilaya ndogo ya Tumbatu kwenye sherehe hizo.
IMG_2359
Afisa Tawala wa Wilaya Ndogo ya Tumbatu ambae pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Redio hiyo Ndg. Mohd Omar Hamad (mwenye suti ya kijivu) akiutambulisha Uongozi na wafanyakazi wa Redio Jamii ya Tumbatu kwa mgeni rasmi makamu wa Rais wa Pili Zanzibar Balozi Sefu Ali Iddi (hayupo pichani)
IMG_2477
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Kaimu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa (Unesco) Bw. Abdul Wahab Coulibaly wakiondoka eneo la tukio mara baada ya kuzindua rasmi redio jamii ya Tumbatu.
IMG_2482
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Issa Mlingoti (kushoto) akibadilishana mawazo na Afisa Mipango Taifa wa Kitengo cha Mawasiliano na Habari na mratibu wa miradi ya UNESCO Yusuph Al-Amin mara baada kumalizika kwa sherehe za uzinduzi wa redio jamii wilaya ndogo ya Tumbatu visiwani Zanzibar.(Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ na Zainul Mzige wa MOblog).

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...