Kuna haja ya kuongeza ukubwa wa eneo, ama kupandisha bei za viingilio ili kuepuka msongamano ndani ya viwanja vya Ngome Kongwe pindi msimu wa Tamasha la kimataifa la Sauti za Busara utakapowadia tena hapo mwakani kutokana na kiwango kikubwa cha mahudhurio kinyume na ilivyotarajiwa.
Tofauti na miaka iliyopita, tamasha la mwaka huu lilitawaliwa sana na wageni, kutoka Tanzania Bara, Afrika Mashariki na Bara la Ulaya, hali ambayo ilisababisha hata upatikanaji wa malazi kwa wageni na usafiri wa kuingia Zanzibar kuwa wa taabu sana, na hata bei za vyakula kuwa juu zaidi tofauti na miaka iliyopita.
Likiwa ni tamasha la sita kufanyika, tangu kuanzishwa kwake, mwanzoni kulikuwa na shaka kwamba huenda lisifanikiwe mwaka huu kutokana na ushiriki mchache wa wasanii wa muziki wa kizazi kipya wa nyumbani, ambapo mwanamuziki pekee wa Hip Hop kutoka nyumbani Joh Makini ndio aliwakilisha muziki wa nyumbani lakini mambo yalikwenda kinyume.
Hii labda ilikuwa ni kutokana na kuhudhuriwa na wadau wengi wa burudani kutoka Ulaya, kikundi kama Segere Original kutoka Tanzania Bara, Cultural Music Troupe, Oudaden kutoka Morocco na Bi Kidude kutoka Zanzibar ambaye alizindua pia filamu ya maisha yake inayoitwa As Old as my tongue walionekana kutia fora kupitiliza.
Ukumbi wa Ngome Kongwe ambao una kawaida ya kuingiza watu 2500, ulionekana kujaa mara mbili ya kawaida ambapo wakazi wa Zanzibar ambao ni nadra sana kupata burudani walilazimika kuingia mapema ukumbuni, takriban masaa mawili kabla ya onesho kuanza ili kupata mahala pazuri pa kukaa patakapowawezesha kuangalia onesho kwa umakini zaidi.
Bi Kidude ambaye mwaka huu kwa mara ya kwanza alipanda jukwaani akiwa amevaa viatu, alikonga nyoyo za mashabiki wake ambao si kwa rika, wala jinsia, uwanja mzima walionekana kumfurahia tofauti na muziki wa kizazi kipya ambao walionekana kulazimisha mashabiki kupiga kelele na makofi, jambo ambalo lilidhihirisha kutofanikiwa kwao.
Tamasha, linatarajiwa kumalizika jumanne ambapo kutakuwa na Full Moon Party, ambapo watu mbali mbali kutoka nchi mbali mbali wanatarajiwa kuonesha uwezo wao katika kupiga muziki.
No comments:
Post a Comment