Tuesday, February 03, 2009
Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika
KIONGOZI wa Libya, Muammar Gaddafi, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa kwa mwaka mzima na Rais Jakaya Kikwete.
Gaddafi, mmoja wa viongozi wakongwe Afrika, akiwa amekaa madarakani kwa takriban miaka 40 tangu alipoingia madarakani kwa mapinduzi yasiyo ya kumwaga damu mwaka 1969, akiwa na miaka 27 tu, alichaguliwa kushika wadhifa huo wa juu AU na viongozi wakuu wa nchi 53, katika mkutano wa 12 wa umoja huo unaofanyika nchini Ethiopia.
Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Elizabeth Blunt, aliyeko kwenye mkutano huo, alikuelezea kuchaguliwa kwa kiongozi huyo msoshalisti, kuwa tukio lililowagawa viongozi wa AU katika makundi mawili, moja ya kundi likimuunga mkono, wakati jingine likionyesha kutoridhishwa na kuchaguliwa kwake.
Kanali Gaddafi anaingia madarakani kwa kipindi cha mwaka mmoja, akiwa mmoja wa viongozi ambao katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa mstari wa mbele kupigania muungano wa nchi za Afrika, wenye lengo la kuunda serikali moja, akiita ‘United States of Africa’, yenye sarafu moja na jeshi moja.
Vyombo vya habari vya nchi za Ulaya Magharibi, vinamtaja Gaddafi kuwa mmoja wa viongozi wajanja na wepesi wa kubadili mwelekeo kwa nia ya kujenga mahusiano mema ya kidiplomasia, kwa kuzingatia matakwa ya wakati.
Kiongozi huyo anakumbukwa kwa namna alivyotokea kuwa mmoja wa maadui wa nchi za Magharibi na Marekani hadi mwaka 2003, wakati alipoamua kusitisha mpango wake wa kuendelea kutengeneza silaha za sumu, hatua ambayo ilisababisha jumuiya ya kimataifa kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Libya.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa AU, Habiba Mejri-Sheikh, jana, ilieleza kwamba, kiongozi huyo wa Libya ambaye uongozi wake umekabiliana na matatizo mbalimbali ya kidiplomasia ambayo wakati fulani yalisababisha taifa lake litengwe kimataifa kabla ya mambo kubadilika, aliwahutubia wakuu wa AU kueleza mwelekeo wa uongozi wake katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.
“Sasa hivi (jana jioni) anahutubia mkutano kama mwenyekiti kuelezea programu na matarajio yake,” alisema msemaji huyo wa AU.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...
-
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu na timu ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa akiwa katika ...
-
NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL OF TANZANIA PSLE-2014 EXAMINATION RESULTS ARUSHA DAR ES SALAAM DODOMA IRINGA KAGERA KIGOMA ...
-
Adam Malima James Wanyancha Hamis Kagasheki RAIS Jakaya Kikwete ameteua Baraza la Mawaziri, huku likiwa na sura na damu mchanganyiko. Bar...
No comments:
Post a Comment