Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, amefanya kikao kazi na Menejimenti ya Wizara hiyo kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji kazi katika sekta ya ardhi ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kikao hicho muhimu kimefanyika leo, Julai 15, 2025, katika Ofisi za Wizara zilizopo Mtumba, Mji wa Serikali, Jijini Dodoma, ambapo viongozi waandamizi wa Wizara wamehudhuria.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mheshimiwa Waziri Ndejembi amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji, ufanisi, na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma kwa wananchi. Amesema kuwa sekta ya ardhi ni nyeti kwa maendeleo ya Taifa na hivyo inapaswa kuendeshwa kwa weledi, uwazi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
“Tunapaswa kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa na Wizara ya Ardhi zinakuwa za haraka, sahihi, na zinazoendana na matarajio ya wananchi. Ucheleweshaji wa huduma na urasimu havina nafasi katika serikali ya awamu ya sita,” alisema Waziri Ndejembi.
Aidha, Waziri amewataka viongozi wa wizara hiyo kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hasa katika kuhuisha ramani, kutoa hatimiliki, kusimamia migogoro ya ardhi, pamoja na kuongeza ushirikiano na Mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau wengine.
Kwa upande wake, Makamishna Wasaidizi, pamoja na Wakurugenzi wa Idara mbalimbali, wamewasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu yao na kuahidi kufanyia kazi mapendekezo na maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri.
Kikao hiki ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuhakikisha sekta ya ardhi inachangia kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wananchi, pamoja na kuvutia uwekezaji kupitia mazingira bora ya umiliki na matumizi ya ardhi.
No comments:
Post a Comment