Dar es Salaam, Julai 12, 2025 — Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, leo amehitimisha mgogoro uliodumu kati ya Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Manzese na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, uliosababishwa na mvutano kuhusu malipo ya Ushuru wa Huduma maarufu kama Service Levy.
Mgogoro huo uliibuka baada ya wafanyabiashara hao kushindwa kulipa ushuru huo kwa mujibu wa sheria, hali iliyowalazimu kufunga maduka 11 kwa siku kadhaa huku wakishinikiza Serikali ianzishe mfumo wa malipo ya ushuru huo kwa kiwango cha pamoja (flat rate), badala ya kutumia mfumo wa asilimia ya mapato.
Katika kikao kilichofanyika leo kati ya uongozi wa Mkoa, Halmashauri ya Ubungo, na wawakilishi wa wafanyabiashara hao, Mhe. Chalamila ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inawathamini sana wafanyabiashara na itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, RC Chalamila alieleza kuwa Ushuru wa Huduma ni wa kisheria na hauwezi kubadilishwa kwa shinikizo la mara moja bila kupitia taratibu za kisheria na ushauri kutoka kwa wizara husika. "Ushuru huu uko kwenye sheria, hatuwezi kubadili sheria kwa haraka namna hiyo, ni lazima mchakato wa kisheria ufuatwe kwa kushirikisha wizara na mamlaka zinazohusika," alieleza Chalamila.
Kwa kuzingatia hali halisi ya baadhi ya wafanyabiashara kushindwa kulipa kwa wakati, Mkuu wa Mkoa amewashauri kuandika maombi rasmi ya kupewa muda maalum wa kukamilisha deni la ushuru huo. Alisisitiza kuwa timu ya wataalam wa biashara itakutana na kila mfanyabiashara mmoja mmoja ili kuona namna bora ya kuwalipisha deni hilo bila kuathiri mwenendo wa biashara zao.
Aidha, RC Chalamila alitoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaoendeleza tabia ya uanaharakati na migomo isiyo na tija kwenye sekta ya biashara. "Biashara ni ya mtu mmoja mmoja, si ya vikundi. Migomo haina tija, inaleta hasara kwa wafanyabiashara wenyewe na kwa uchumi wa mtaa na jiji kwa ujumla. Tusiige uanaharakati usiofaa katika masuala ya uchumi," alisisitiza.
Katika hatua ya mwisho ya kikao hicho, wafanyabiashara wa Manzese waliridhia kufungua maduka yao na kurejea katika shughuli zao kama kawaida. Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, baadhi ya viongozi wa jumuiya hiyo walimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa usikivu, hekima, na njia ya majadiliano aliyoitumia kumaliza mvutano huo.
No comments:
Post a Comment