Comoro, Julai 6, 2025 —
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza dhamira ya Tanzania kuendeleza na kuimarisha mahusiano ya kidugu kati ya Tanzania na Muungano wa Visiwa vya Comoro. Akiwa nchini humo kushiriki maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Comoro, Rais Samia amesema uhusiano huo hautaishia kwenye misingi ya kidiplomasia pekee bali utaendelea kwa moyo wa ujamaa, amani, lugha ya Kiswahili, na mshikamano wa kweli wa Kiafrika.
Akihutubia katika Uwanja wa Malouzini Omnisport mjini Moroni, Rais Samia amesema Tanzania itaendeleza ushirikiano wa kiuchumi, kijamii, mazingira na diplomasia, kama sehemu ya kujenga Afrika imara kupitia urafiki wa kweli na majirani zake.
Rais Samia amekumbusha namna Tanzania ilivyoshiriki harakati za ukombozi kwa nchi mbalimbali za Afrika, ikiwemo Comoro, kwa kutoa hifadhi, msaada wa kifedha, kisiasa na kiulinzi kwa wapigania uhuru. Amewataja pia wanawake mashujaa wa Tanzania waliotoa mchango katika ukombozi huo.
Akiwapongeza wananchi na serikali ya Comoro, Rais Samia amesema taifa hilo limepiga hatua kubwa katika sekta ya uchumi, miundombinu, afya, elimu, utalii na huduma za jamii. Amempongeza Rais wa Comoro, Mhe. Azali Assoumani, kwa kuwa kiongozi mwenye maono makubwa katika maendeleo.
Katika kuimarisha mahusiano ya kiuchumi, Rais Samia ametangaza mikakati ya kukuza usafiri kati ya Tanzania na Comoro kupitia mashirika ya ndege ya Air Tanzania na Precision Air, pamoja na usafiri wa majini, hatua ambayo inalenga kukuza biashara na muingiliano wa watu wa mataifa haya mawili.
Amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na Comoro katika kufundisha lugha ya Kiswahili mashuleni, kulinda mazingira ya Bahari ya Hindi, na kuwezesha miradi ya maendeleo kupitia taasisi kama Benki ya Exim, Benki ya Wajasiriamali Vijana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambazo tayari zina mpango wa kupanua huduma zake nchini Comoro.
Kwa kumalizia, Rais Samia ametoa rai kwa wananchi wa Comoro kuenzi uhuru wao kwa kujenga mshikamano, haki na usawa ili kufikia maendeleo jumuishi. Ameahidi kwamba Tanzania itaendelea kuwa bega kwa bega na Comoro katika safari ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment