Saturday, July 05, 2025

MAKAMU WA RAIS MHE. DKT. MPANGO ASHIRIKI MISA YA UPADIRISHO NA UFUNGUZI WA MWAKA WA JUBILEI YA MIAKA 50 KIWANJA CHA NDEGE, DODOMA














Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameungana na waumini pamoja na viongozi mbalimbali wa Kanisa Katoliki kushiriki katika Misa Takatifu ya Upadirisho na Uzinduzi wa Mwaka wa Jubilei ya Miaka 50 ya Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska iliyopo Kiwanja cha Ndege, mkoani Dodoma.

Misa hiyo imeongozwa na Mhashamu Askofu Beatus Kinyaiya, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, ambapo aliwataka waumini kutumia fursa ya mwaka huu wa uchaguzi kwa kupiga kura kwa amani na kuwachagua viongozi watakaoitumikia jamii kwa uadilifu katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Katika mahubiri yake, Askofu Kinyaiya pia ameonya juu ya matumizi mabaya ya akili mnemba (AI), akisisitiza kuwa teknolojia hiyo itumike kwa faida ya jamii na si kwa kueneza maovu na udanganyifu.

Wakati wa Misa hiyo, Mashemasi watatu walipadrishwa kuwa Mapadre wa Kanisa Katoliki, akiwemo Padre Joseph Ibrahim, Padre Sajilo Mark, na Padre Damian Mtanduzi.

Aidha, tukio hilo limehudhuriwa na waumini kutoka maeneo mbalimbali na kuambatana na uwekaji wa jiwe la msingi la jengo jipya la Katekesi, litakalotumika kwa ajili ya kufundishia mafundisho ya dini katika parokia hiyo.

Sherehe hiyo imebeba maana kubwa ya kiroho, kihistoria na kijamii, ikielezea ukuaji wa Parokia hiyo kwa kipindi cha nusu karne na kuimarisha maadili ya kiimani kwa jamii ya Kiwanja cha Ndege na maeneo jirani.

No comments:

VIONGOZI WA MANISPAA YA KIBAHA WATEMBELEA MBUGA YA MIKUMI KUUNGA MKONO UTALII WA NDANI

  Mikumi, Morogoro – Katika juhudi za kuunga mkono kampeni ya kukuza utalii wa ndani iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanza...