Monday, July 14, 2025

WAZIRI CHANA AKABIDHI VIFAA VYA KISASA KUKABILIANA NA UJANGILI VYENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 240



Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri Wa Maliasili Na Utalii Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb), amepokea na kukabidhi vifaa vya kisasa vya kusaidia kupambana na kudhibiti ujangili na kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kutoka kwa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara haramu wa (IWT).

Akizungumza jijini Dodoma leo 14 Julai, 2025 wakati wa hafla fupi wa makabidhiano hayo, Waziri Chana amesema vifaa hivyo vya doria vyenye thamani ya  Dola za Kimarekani 91,000 sawa na  shilingi za Kitanzania millioni 240 na vimekuwa chachu katika juhudi za Serikali za kupambana na ujangili hapa nchini.

“Leo hii tunapokea vifaa (Pikipiki 20 na Ndege Nyuki (Drones) 07) kwa ajili ya Kupambana na Ujangili na Biashara haramu ya Nyara, Vifaa hivi ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi huu na niwatake mkavitumie katika kuimarisha shughuli za uhifadhi na kudhibiti ujangili katika maeneo yenu” alisema Waziri Chana.

Aidha, Mhe. Chana ametaja manufaa ya utekelezaji wa Mradi huo ikiwa ni pamoja na kuwezesha juhudi za Serikali katika kudhibiti ujangili wa Tembo ambapo idadi yao imeongezeka  kutoka 43,000 mwaka 2014 hadi kufikia zaidi ya 60,000 mwaka 2022.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt.  Fortunata Msoffe ameseama Mradi  huo wa IWT pia umechangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha Vikundi vya Kuratibu Doria (TCGs) kwenye Kanda za Kiikolojia, kutoa Mafunzo kwa Askari na Maafisa wa Uhifadhi, kuwezesha matumizi ya Taarifa za Kiintelijensia, pamoja na Kuimarisha Ushirikiano wa Taasisi mbalimbali za Ulinzi na Uhifadhi.

“Mradi huu unaendelea kutekeleza miradi ya kupunguza migogoro kati ya Binadamu na Wanyamapori na kuchangia kuboresha maisha ya jamii kupitia njia ya uwezeshaji wa shughuli za kuongeza kipato kama vile Ufugaji Nyuki, Kilimo cha Mazao yasiyopendwa na Wanyamapori kwa kuzingatia usawa wa Kijinsia na Ushirikishwaji wa Jamii husika.” Alisema Dkt. Msoffe.

Naye, Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Godfrey Mulisa, amesema ufadhili wa vifaa hivyo kwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara hiyo ni kutokana na kufurahishwa na juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii na kukabiliana na ujangili na biashara haramu.

No comments:

WAZIRI CHANA AKABIDHI VIFAA VYA KISASA KUKABILIANA NA UJANGILI VYENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 240

Na Mwandishi Wetu, Dodoma Waziri Wa Maliasili Na Utalii Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb), amepokea na kukabidhi vifaa vya kisasa vya kusai...