KIGOMA: Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mradi wa Kuboresha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP), imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 5.7 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule mbili mpya za sekondari mkoani Kigoma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza upatikanaji na ubora wa huduma za elimu kwa wanafunzi wa kike na wale wanaohitaji elimu ya amali.
Miongoni mwa shule hizo ni Shule ya Sekondari ya Wasichana Kigoma, iliyojengwa katika Wilaya ya Uvinza. Shule hiyo tayari imeanza kutoa huduma za elimu na imejengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 4.1. Miundombinu iliyojengwa katika shule hiyo ni pamoja na:
-
Maabara za masomo
-
Vyumba vya madarasa na ofisi
-
Mabweni ya wanafunzi
-
Vyoo vya walimu na wanafunzi
-
Nyumba za walimu
-
Jengo la utawala
-
Bwalo la chakula
-
Jengo la TEHAMA
-
Mashimo ya maji taka
Katika hatua nyingine, Serikali inaendelea na ujenzi wa Shule mpya ya Amali katika Wilaya ya Kibondo, mkoani Kigoma, kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.6. Shule hii ya kisasa inalenga kuwapatia wanafunzi elimu ya amali na mafunzo ya stadi za kazi, ikiwa ni utekelezaji wa Sera mpya ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, toleo la mwaka 2023.
Hatua hizi ni ushahidi wa dhamira ya Serikali kuboresha mazingira ya ujifunzaji, kuongeza fursa za elimu kwa wasichana na vijana, pamoja na kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
No comments:
Post a Comment