Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongoza Kikao cha mwisho cha Baraza la Mawaziri cha Serikali ya Awamu ya Sita kilichofanyika tarehe 14 Julai, 2025 katika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.
Kikao hicho cha kihistoria kimekusanya pamoja Mawaziri, Makatibu Wakuu na viongozi wengine wakuu wa Serikali kwa ajili ya kufanya tathmini ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita, kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Viongozi hao walifika Ikulu Chamwino mapema asubuhi kwa ajili ya kushiriki kikao hicho cha mwisho, ambacho kimeangazia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Awamu ya Sita, changamoto zilizojitokeza, na maelekezo ya kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali kuelekea uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Kikao hicho pia kimetoa nafasi kwa Rais kutoa shukrani kwa Mawaziri na viongozi wote kwa ushirikiano waliompa katika kipindi cha uongozi wake, na kueleza dhamira ya kuendeleza kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya Watanzania wote.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu, kikao hiki ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa Serikali wa kutathmini hatua zilizofikiwa katika kutekeleza mipango ya maendeleo, pamoja na kuweka mikakati ya muda mfupi na mrefu ya kusimamia mabadiliko yanayotarajiwa baada ya uchaguzi mkuu.
No comments:
Post a Comment