Thursday, July 24, 2025

*KAMISHNA KUJI AKAGUA ENEO LA KOGATENDE SERENGETI ASISITIZA MAAFISA NA ASKARI UHIFADHI KUENDELEA KUSIMAMIA SHERIA ZA HIFADHI ILI KUIMARISHA SHUGHULI ZA UTALII












Na. Philipo Hassan - Serengeti

Kamishna wa Uhifadhi, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) CPA Musa Nassoro Kuji, leo Julai 24, 2025 amefanya ukaguzi katika eneo la vivuko vya nyumbu (Kogatende) ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti. Katika ukaguzi huo alielekeza Maafisa na Askari Uhifadhi kusimamia sheria ipasavyo, taratibu na miongozo mbalimbali ya Hifadhi za Taifa ili kuboresha shughuli za utalii endelevu usioharibu mazingira.

Ziara ya Kamishna Kuji ni muendelezo wa ziara zake za kikazi kukagua shughuli za maendeleo na utekelezaji wa miongozo mbalimbali iliyowekwa na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuwa na uhifadhi endelevu ambao ndio kiini cha utalii tunaoushuhudia leo ukilipatia Shirika na Taifa mapato na fedha za kigeni ambazo zimeendelea kuchagiza katika uchumi wa Taifa letu.

Akizungumza katika ziara hiyo Kamishna Kuji alitoa maagizo kwa Maafisa na Askari Uhifadhi wanaosimamia shughuli za utalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kuendelea kusimamia sheria, kanuni na taratibu zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuboresha huduma bora kwa watalii na kuwakumbusha kuzifuata ili kuondoa mkanganyiko wa mara kwa kwa mara. 

Aidha, Kamishna Kuji alisema, “Endeleeni kuchukua tahadhari na kuendelea kusimamia taratibu na sheria za hifadhi zilizowekwa kwa ajili ya kudhibiti vitengo vya uvunjifu wa sheria na miongozo ya hifadhi iliyowekwa. Kuweni imara kudhibiti matendo yanayokiuka taratibu zote za kiuhifadhi zinazofanywa na waongoza utalii wasio na weledi kama vile kushusha watalii kwenye  magari maeneo yasiyoruhusiwa ambayo ni hatari kwa watalii na waongoza watalii pia”.

Vilevile, CPA Kuji aliongeza, Simamieni na kuthibiti magari yanayotumia njia zisizo halali na rasmi  “Offroading”, kutupa taka hifadhini, mwendokasi na tabia ya kulisha wanyamapori, kwa wale watakaokengeuka na kutotii sheria na taratibu hizo, sheria ichukue mkondo wake”.  

Naye, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Stephano Msumi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti akitoa taarifa ya tukio lililotokea Julai 21, 2025 ambapo picha jongefu na mnato zilionekana katika mitandao ya kijamii zikionesha watalii wakiwa wameshuka kutoka kwenye magari

katika eneo la Kogatende kivuko namba nne wameshajulikana na taratibu za adhabu zinaendelea kuchukuliwa kwa kufuata miongozo na hatutamuonea mtu wala kumfumbia mtu macho.

“ Hata hivyo, Afande Kamishna, kama hifadhi hii mama na yenye watalii wengi tumeshachukua hatua kali za kisheria kutokana na tukio hilo ambapo kampuni zote zilizohusika kuvunja sheria na taratibu kwa kushusha watalii kutoka kwenye magari yao katika maeneo ambayo hayaruhusiwi tayari zimeanza kuchukuliwa”, alisema Mhifadhi Msumi.

Kamishna Msumi aliongeza kuwa “Ni jukumu la kila mmoja wetu kwa maana ya TANAPA, waongoza watalii, madereva pamoja na wadau wote wa utalii kuhakikisha kuwa tunafuata sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa tuwapo hifadhini ili kuendelea kutunza maliasili zetu ambazo ni chanzo cha kuleta watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani.  Na watalii hao hukuza uchumi wa watanzania pamoja na kuchangia kuongeza pato la Taifa.

Katika kuhitimisha ziara yake Kamishna Kuji ametoa maelekezo kwa uongozi wa Kanda ya Magharibi na Hifadhi ya Taifa Serengeti kuongeza nguvu katika kuimarisha shughuli za ulinzi na usalama katika eneo la Nyatwali Wilayani Bunda ambalo Shirika limekabidhiwa kwa ajili ya kulijumuisha kuwa sehemu ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa manufaa ya shughuli za uhifadhi na utalii hapa nchini. ‎

No comments:

*KAMISHNA KUJI AKAGUA ENEO LA KOGATENDE SERENGETI ASISITIZA MAAFISA NA ASKARI UHIFADHI KUENDELEA KUSIMAMIA SHERIA ZA HIFADHI ILI KUIMARISHA SHUGHULI ZA UTALII

Na. Philipo Hassan - Serengeti Kamishna wa Uhifadhi, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) CPA Musa Nassoro Kuji, leo Julai 24, 2025...