Monday, July 14, 2025

MCL YAMUOMBA RADHI NEHEMIA KYANDO MCHECHU




UONGOZI wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), wachapishaji wa magazeti ya MwananchiThe Citizen na Mwanaspoti, umeomba radhi kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Msajili wa Hazina wa sasa, Bw. Nehemia Kyando Mchechu, kufuatia taarifa za upotoshaji zilizochapishwa katika gazeti la The Citizen.

Radhi hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama ya Rufani Tanzania wa Juni 4, 2025, ambapo maombi ya rufaa yaliyowasilishwa na MCL dhidi ya Mchechu yalitupiliwa mbali, na hivyo kuithibitisha hukumu ya awali ya Mahakama Kuu iliyotolewa Machi 3, 2023.

Katika hukumu hiyo, The Citizen iliamriwa kumlipa Mchechu fidia ya shilingi bilioni 2.5 kutokana na taarifa ya Machi 23, 2018 iliyokuwa na kichwa cha habari “Kwa nini JPM alivunja Bodi ya NHC na kumng’oa Mchechu?”, iliyobainika kuwa ya uongo na isiyo na ushahidi wowote.

Mahakama pia iliagiza radhi hiyo kuchapishwa ukurasa wa mbele kwa ukubwa sawa na habari ya awali, na kulipa riba ya asilimia 12 kwa mwaka endapo fedha hiyo haitalipwa kwa wakati. Aidha, ilizitaka The Citizen kuepuka kuchapisha taarifa za uongo kuhusu Mchechu bila ushahidi wa kutosha.

Taarifa hiyo ya awali ilidai kuwa Mchechu alikuwa akichunguzwa na Bodi ya NHC na TAKUKURU kuhusu miradi ya Safari City – Arusha, mradi wa Kawe na tuhuma nyingine zisizothibitishwa, ikiwemo mgongano wa kimaslahi na matumizi mabaya ya madaraka.

Hata hivyo, Mahakama ilibaini kuwa ushahidi uliotolewa na The Citizen haukuthibitisha madai hayo, na hivyo Mchechu akahukumiwa kushinda kesi hiyo na kutunukiwa fidia pamoja na hadhi yake kurejeshwa.

Kwa uamuzi huo wa Mahakama ya Rufani, MCL imetekeleza agizo la kuomba radhi, hatua iliyopongezwa na wengi kama ishara ya kuwajibika na kuheshimu utu wa mtu pamoja na misingi ya haki.


No comments:

VIONGOZI WAKUU WA SERIKALI WAPIGA PICHA YA PAMOJA BAADA YA KIKAO CHA MWISHO CHA BARAZA LA MAWAZIRI AWAMU YA SITA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongoza kikao cha mwisho cha Baraza la Mawaziri cha Serikali...