MEATU, SIMIYU – Juni 17, 2025:
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu kwa kushiriki mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya stendi ya mabasi wilayani Meatu.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Meatu na mikoa ya jirani, Rais Samia aliwasilisha taarifa ya mafanikio mbalimbali ya Serikali ya Awamu ya Sita na kueleza mikakati kabambe ya kuleta maendeleo endelevu katika maeneo ya vijijini na mijini.
Akihutubia wananchi kwa hamasa kubwa, Rais Samia aliwahakikishia wananchi wa Meatu kuwa Serikali inaendelea kuweka mkazo katika utekelezaji wa miradi ya maji, barabara, afya, elimu na kilimo ili kuinua uchumi wa wananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
"Serikali yenu ipo kazini na tutaendelea kusogeza huduma karibu na wananchi. Maendeleo hayachagui rangi, dini wala kabila – bali yanafuata mahitaji halisi ya watu," alisema Rais Samia huku akishangiliwa na wananchi waliokuwa na mabango yenye ujumbe wa shukrani na matumaini.
SHAMRASHAMRA ZATIKISA MEATU
Shangwe, nderemo na vifijo vilitawala uwanja huo huku wananchi wakionesha furaha yao kwa ujio wa Rais Samia, wakisema ni mara ya kwanza kwa viongozi wa juu wa kitaifa kufika na kusikiliza changamoto zao moja kwa moja.
Vikundi vya burudani vilipamba tukio hilo kwa ngoma za asili, nyimbo na maigizo yenye ujumbe wa kuhamasisha maendeleo na mshikamano wa kitaifa.
Wananchi wengi walieleza kufurahishwa na namna Rais Samia anavyowajali na kushughulikia changamoto zao, huku wakiahidi kuendelea kumuunga mkono katika juhudi zake za kuijenga Tanzania mpya yenye usawa, maendeleo na ustawi kwa wote.
Ziara ya Rais Samia mkoani Simiyu inaendelea na imejikita katika kukagua miradi ya maendeleo, kuzungumza na wananchi, pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.
No comments:
Post a Comment