Na Mwandishi Wetu, Kisarawe – Pwani
Ujumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetembelea Hifadhi za Mazingira Asilia za Pugu–Kazimzumbwi na Vikindu mkoani Pwani, ukielezea kuridhishwa na kasi ya uwekezaji wa miradi ya uhifadhi na utalii wa ikolojia inayoendelea kutekelezwa na TFS.
Ziara hiyo ya siku mbili, iliyoanza tarehe 24 Juni 2025, iliongozwa na Mjumbe wa Bodi, Bi Piencia Kiure, ikiwa ni sehemu ya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi na maendeleo ya utalii katika maeneo ya hifadhi za misitu ya asili, ambayo ni muhimu kwa bioanuwai na huduma za kiikolojia.
Akizungumza katika ziara hiyo, Bi Kiure alieleza kufurahishwa na uboreshaji wa miundombinu ya hifadhi hizo, hususan katika maeneo ya kupokelea wageni, vibanda vya mapumziko na ukumbi wa shughuli za kijamii na kitalii.
"Ni dhahiri sasa kwamba hata Mkoa wa Pwani unaweza kuwa kitovu cha utalii wa misitu. Hifadhi ya Pugu–Kazimzumbwi na Vikindu ni maeneo ya pekee kwa utalii wa kimya, kutafakari, na kutuliza akili. Huu ni utalii unaomgusa moja kwa moja binadamu katika afya ya akili na ustawi wa jamii,” alisema Bi. Kiure.
Aidha, alisisitiza kuwa uwekezaji unaoendelea kufanywa na TFS chini ya uongozi wa Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, ni ishara ya utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kuongeza mchango wa sekta ya misitu katika uchumi wa Taifa kupitia uhifadhi endelevu na utalii wa mazingira.
"Bodi inatambua juhudi kubwa zinazofanywa na menejimenti ya TFS. Kasi ya utekelezaji wa miradi ni ya kutia moyo na tunaamini itaongeza idadi ya watalii wa ndani na nje ya nchi, sambamba na kuimarisha mapato ya serikali na huduma kwa jamii,” aliongeza.
Kwa upande wake, Kamanda wa Kanda ya Mashariki wa TFS, Bw. Mathew Ntilicha, aliyemwakilisha Kamishna wa Uhifadhi, aliishukuru Bodi kwa ziara hiyo na kupokea mapendekezo yaliyotolewa kwa ajili ya kuboresha zaidi maeneo ya hifadhi.
"Tunaendelea kuboresha huduma, kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii zinazozunguka hifadhi, na kuandaa vivutio vya kipekee vitakavyovutia wageni wa ndani na wa kimataifa. Tunawakaribisha Watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali kutembelea maeneo haya,” alisema Ntilicha.
Wakati wa ziara hiyo, wajumbe wa Bodi walitembelea pia baadhi ya miradi ya kimkakati ikiwemo ule wa “Kuimarisha Ustahimilivu wa Bioanuwai ya Misitu ya Mazingira Asilia dhidi ya Matishio ya Mabadiliko ya Tabianchi,” unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF).
Katika ziara hiyo, ujumbe wa Bodi ulipata fursa ya kukutana pia na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mh. Petro Magoti, ambaye alipongeza juhudi za TFS katika kulinda rasilimali za taifa.
"Uwepo wa ugeni huu ni ishara ya dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za umma. Juhudi za TFS katika uhifadhi ni mfano bora wa utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema DC Magoti.
Ziara ya wajumbe wa Bodi ya TFS inatarajiwa kuhitimishwa leo tarehe 25 Juni 2025, ambapo wajumbe watakutana na Menejimenti ya TFS Kanda ya Mashariki kwa ajili ya majadiliano ya kitaalamu, tathmini ya miradi, na kutoa maelekezo ya kimkakati kwa maboresho ya baadaye.
No comments:
Post a Comment