Simiyu, 18 Juni 2025
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameweka jiwe la msingi katika Shule ya Sekondari ya Amali ya Mwamapalala iliyopo wilayani Itilima, mkoani Simiyu, kwa niaba ya shule zote 103 za Sekondari za Amali zinazojengwa nchini kote.
Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wananchi pamoja na wanafunzi wa shule hiyo, ambapo Mhe. Rais Samia amesisitiza umuhimu wa elimu ya amali katika kujenga taifa lenye ujuzi wa vitendo na uwezo wa kushindana katika soko la ajira.
"Shule hizi za Amali ni mkombozi kwa vijana wetu. Zinatoa maarifa ya darasani pamoja na stadi za maisha, jambo litakalowawezesha kujiajiri na kuchangia maendeleo ya taifa," alisema Rais Samia.
Katika hatua nyingine ya kukuza uchumi wa viwanda, Mhe. Rais Samia pia amezindua rasmi Kiwanda cha kuchakata pamba cha Shree Rajendra Agro Industries Limited kilichopo wilayani Maswa, mkoani Simiyu. Kiwanda hicho ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, hasa pamba, inayolimwa kwa wingi katika kanda ya ziwa.
Rais Samia amesema uzinduzi wa kiwanda hicho ni hatua muhimu kuelekea Tanzania ya viwanda, na kwamba Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kukuza ajira, kuongeza mapato na kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi.
Ziara ya Rais Samia mkoani Simiyu inaonyesha dhamira yake ya dhati katika kuimarisha sekta ya elimu, viwanda na kuinua maisha ya Watanzania kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment