Friday, June 20, 2025

SERIKALI YA ZANZIBAR YAIPONGEZA TANAPA KWA KUKUZA USHIRIKIANO NA KUBORESHA UTALII





Na. Mwandishi wetu - Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale imeipongeza TANAPA kwa ushirikiano mkubwa unaoendelea kuoneshwa katika kuendeleza sekta ya utalii na kuhifadhi urithi wa Taifa, kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Utalii na Uwekezaji yanayofanyika katika viwanja vya Dimani Fumba, Zanzibar.

Akizungumza leo Juni 20, 2025 Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga, alisema TANAPA kupitia Ofisi Kiunganishi ya Zanzibar imekuwa mfano bora wa taasisi inayoshirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii, na kuwa cheti cha heshima walichotunukiwa ni alama ya kutambua mchango wao katika kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo.

Awali, akiongea kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Fredrick Malisa anayeshughulikia Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Kanda ya Mashariki, alisema shirika linaendelea kujipambanua kama mdau mkuu katika kukuza utalii endelevu na kuvutia uwekezaji katika Hifadhi 21 za Taifa. Alisisitiza kuwa maonesho haya yamekuwa jukwaa muhimu kwa TANAPA kuwasiliana moja kwa moja na wawekezaji na kuwakaribisha kushirikiana katika katika kutambua fursa za utalii na uwekezaji. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Ofisi Kiunganishi ya TANAPA Visiwani  Zanzibar, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Halima Kiwango, alieleza kuwa TANAPA imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kushirikiana na Serikali na wadau kwa kutoa taarifa ya vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi za Taifa, fursa za uwekezaji na huduma kwa watalii sanjari na mazao ya utalii. 

Naye mdau wa utalii kutoka Zanzibar, Sabra Saleh, alisema ushiriki wa TANAPA katika maonesho hayo umeleta hamasa kubwa kwa vijana na wadau wa ndani kuingia kwenye sekta ya utalii. Alisema Shirika linaonesha mwelekeo mzuri wa utalii wa asili unaojengwa katika misingi ya ushirikiano na maendeleo kwa jamii.

Kwa ujumla, ushiriki wa TANAPA katika maonesho haya ni kielelezo cha dhamira ya Shirika hilo kuendelea kushirikiana na wadau wote wa maendeleo ndani na nje ya nchi, katika kulinda urithi wa Taifa, kukuza utalii endelevu na kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye maendeleo ya uchumi wa Taifa kupitia uhifadhi na Utalii.

No comments:

SERIKALI YA ZANZIBAR YAIPONGEZA TANAPA KWA KUKUZA USHIRIKIANO NA KUBORESHA UTALII

Na. Mwandishi wetu - Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale imeipongeza TANAPA kwa ushirikian...