Chinangali – Dodoma, 18 Juni 2025
Mkazi wa Nkuhungu Jijini Dodoma, Bi. Azara Dosa, ameonesha furaha na kuridhishwa kwake na huduma zinazotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, hususan katika eneo la utoaji wa hatimiliki na usimamizi wa sekta ya ardhi kwa uwazi na weledi wa hali ya juu.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa hatimiliki ya kiwanja chake katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park, Bi. Azara amesema huduma aliyoipata ni ya kiwango cha juu na ni ushahidi wa dhahiri wa maboresho makubwa yaliyofanywa katika sekta ya ardhi.
“Nimepokea hatimiliki yangu leo na nafurahi sana. Huduma imekuwa ya haraka, wazi, na watumishi wameonesha weledi mkubwa. Kwa kweli nawapongeza sana Serikali na Wizara kwa juhudi hizi,” amesema Bi. Azara kwa furaha.
Huduma za Kliniki ya Ardhi katika maadhimisho hayo zimekuwa kivutio kwa wananchi wengi ambao wanapata nafasi ya kusikilizwa, kupata ushauri wa kitaalamu na kutatuliwa changamoto zao za ardhi papo kwa papo.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ni jukwaa muhimu la Serikali kuwasogelea wananchi na kutoa huduma kwa karibu, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya dhati ya kuimarisha uwajibikaji, uwazi na utumishi uliotukuka kwa maslahi ya umma.
No comments:
Post a Comment