Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, amewasili leo tarehe 25 Juni 2025 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nnamdi Azikiwe uliopo Jijini Abuja, Nigeria, kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa 32 wa Benki ya Maendeleo ya Mauzo ya Nje ya Afrika (Afrexim Bank).
Makamu wa Rais anahudhuria mkutano huo akimwakilisha Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amenominate uwakilishi huo wa juu katika mkutano unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 25 hadi 27 Juni 2025.
Aidha, Watanzania mbalimbali waishio nchini Nigeria walijitokeza kumpokea kwa furaha na heshima Makamu wa Rais alipowasili, wakionesha mshikamano na mapenzi kwa taifa lao. Tukio hilo limeonesha uzito na umuhimu wa ushiriki wa Tanzania katika mikutano ya kikanda na kimataifa yenye lengo la kuimarisha uchumi na ushirikiano wa kibiashara kati ya mataifa ya Afrika.
Mkutano wa Afrexim ni jukwaa muhimu linalokutanisha viongozi wa serikali, sekta binafsi, taasisi za kifedha na wawekezaji kujadili fursa za maendeleo ya biashara barani Afrika, ambapo Tanzania ina nafasi muhimu ya kuchangia na kunufaika.
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huu unatarajiwa kuimarisha zaidi ushirikiano wa kifedha na kibiashara kati ya Tanzania na nchi nyingine wanachama wa Benki ya Afrexim.
No comments:
Post a Comment