Monday, June 09, 2025

BUNGE LAPITISHA MAREKEBISHO YA SHERIA YA SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA (NHC)











Dodoma, Juni 9, 2025 – Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeupitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wa mwaka 2025 katika kikao cha 42 cha mkutano wa 19 wa Bunge la Bajeti kilichofanyika leo jijini Dodoma.

Muswada huo umesomwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi, ambaye alieleza kuwa marekebisho hayo yamelenga kuboresha ufanisi wa Shirika, kuongeza uwajibikaji, na kulifanya lifanye kazi kwa mujibu wa mazingira ya sasa ya kiutendaji na kijamii.

Miongoni mwa vifungu vilivyofanyiwa marekebisho ni vifungu vya 12 na 13, ambavyo vimeondoa wajibu wa mwajiri kukata kodi ya nyumba pamoja na faini ya ucheleweshaji wa kodi moja kwa moja kutoka kwenye mshahara wa mfanyakazi anayeishi kwenye nyumba ya Shirika. Badala yake, wafanyakazi hao watalipa kodi moja kwa moja kama wapangaji wa kawaida. Lengo la hatua hii ni kuongeza uwajibikaji binafsi wa mpangaji na kurahisisha ukusanyaji wa kodi kwa upande wa Shirika.

Kuimarisha Utendaji na Uwajibikaji

Katika kuboresha usimamizi wa Shirika, Bunge pia limepitisha marekebisho ya Kifungu cha 5 kwa kuongeza majukumu mapya kwa Bodi ya Shirika na kuweka masharti ya wazi ya uundwaji wa kamati mbalimbali zitakazosaidia katika utekelezaji wa majukumu ya Bodi kupitia Kifungu kipya cha 5A. Marekebisho haya yanalenga kuongeza ufanisi katika maamuzi na utekelezaji wa mikakati ya Shirika.

Kifungu cha 9 pia kimeboreshwa ili kumpa Mkurugenzi Mkuu uwezo mpana wa kukasimisha mamlaka ya kusaini nyaraka mbalimbali kwa maafisa waandamizi. Awali, mamlaka haya yalihusu tu mikataba ya upangaji, lakini sasa yatahusisha nyaraka nyingine zinazohusiana na majukumu ya Shirika, hatua inayolenga kuharakisha utendaji kazi.

Marekebisho ya Kiutawala na Kisheria

Katika kuhakikisha utawala bora, Kifungu cha 18 kimebadilishwa ili mamlaka ya kumteua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika ihamishiwe kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania badala ya Waziri. Aidha, Kifungu kipya cha 18A kimeongezwa ili kutenganisha masharti ya uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu na ajira za watumishi wengine wa Shirika. Hatua hii inalenga kuweka uwazi na mpangilio bora wa kiutawala.

Kifungu cha 20 kimefanyiwa marekebisho ili kuhakikisha posho na malipo mengine kwa wajumbe wa Bodi yanatolewa kwa mujibu wa miongozo ya Serikali, hatua inayowiana na usimamizi wa fedha za umma. Kifungu cha 21 kimeondoa masharti yanayohusu michango ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuwa tayari yanafafanuliwa katika sheria nyingine husika.

Adhabu kwa Makosa ya Kisheria

Vifungu vya 15, 16, 17 na 32 vimeboreshwa kwa kuongeza viwango vya adhabu dhidi ya mtu au taasisi itakayobainika kutoa taarifa za uongo, kuficha siri za Shirika au kuzuia ukaguzi wa nyumba. Marekebisho haya yanazingatia thamani halisi ya fedha kwa sasa na uzito wa makosa yanayohusika.

Kuboresha Uwekezaji na Chanzo cha Mapato

Bunge pia limeidhinisha marekebisho ya Kifungu cha 23 kwa kuongeza ruzuku kama chanzo rasmi cha mapato ya Shirika, hatua itakayosaidia kuongeza uwezo wa kifedha wa NHC. Vifungu vya 25 na 26 vimefutwa kwa sababu ya kutokutekelezwa kwa muda mrefu na kutokuwa na umuhimu katika shughuli za Shirika. Hii ni pamoja na kuondoa Mfuko wa Dhamana na Mfuko Mkuu wa Akiba.

Marekebisho ya Kifungu cha 24 yameondoa mamlaka ya Bodi kudhamini mikopo kwa niaba ya Shirika ili kuendana na Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada ya Serikali (Sura ya 134). Aidha, Bodi sasa itaruhusiwa kuwekeza bila ya kuhitaji idhini ya Waziri, mradi uwekezaji huo uendane na Sheria ya Msajili wa Hazina (Sura ya 370).

Mikakati ya Kudhibiti Migongano ya Maslahi

Vifungu vya 31 na 31A vimeboreshwa ili kuweka utaratibu wa kushughulikia migongano ya maslahi ndani ya Shirika bila kutegemea rejea ya moja kwa moja kwenye Sheria ya Ardhi. Lengo ni kuhakikisha NHC inatekeleza majukumu yake kwa uadilifu na kwa mujibu wa sheria.

Jedwali la Sheria pia limefanyiwa marekebisho ili kuwiana na taratibu na miongozo ya usimamizi wa mashirika ya umma, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa Bodi na kuimarisha uwajibikaji wake.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisisitiza kuwa marekebisho haya yamezingatia mazingira halisi ya sasa, changamoto za utekelezaji wa sheria ya awali, na hitaji la kuifanya NHC kuwa taasisi inayojitegemea kifedha, yenye uwazi, na inayowajibika ipasavyo kwa wananchi.

Kwa sasa, Shirika la Nyumba la Taifa lina nafasi ya kujiimarisha zaidi na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba bora za makazi, uwekezaji wa kimkakati, na kuchochea maendeleo ya miji nchini.

No comments:

MAJALIWA: FANYENI TAFITI ZENYE TIJA KWA WANANCHI

Dar es Salaam, 18 Juni 2025 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa watafiti na wapangaji wa s...