Mwanza, Juni 20, 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo ameongoza maadhimisho ya kipekee yaliyojumuisha makundi mbalimbali ya walinzi wa jadi (Sungusungu) na bodaboda kutoka mikoa ya Mwanza, Simiyu, Geita, Shinyanga na Tabora, katika uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Makundi hayo yalipita kwa heshima mbele ya Rais Samia katika gwaride lililojaa ujasiri, mshikamano na uzalendo, yakionesha dhamira yao ya dhati katika kulinda amani, mali za wananchi na kushirikiana na vyombo vya dola katika masuala ya ulinzi na usalama wa jamii.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Samia alieleza kuwa Serikali inatambua, kuthamini na kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Sungusungu na vikundi vya ulinzi shiriki nchini kote. Alisema makundi haya yamekuwa na mchango mkubwa hususan katika maeneo ya vijijini ambako ulinzi wa kijamii ni wa msingi.
"Walinzi wa jadi ni sehemu ya mfumo wetu wa jadi wa utatuzi wa migogoro na ulinzi wa kijamii. Serikali itaendelea kuhakikisha wanapata mafunzo ya msingi ya ulinzi na usalama, ili kuboresha utendaji wao kwa kuzingatia sheria za nchi na haki za binadamu," alisema Mhe. Rais Samia.
Aidha, aliwahimiza Sungusungu na bodaboda kuendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi na serikali za mitaa ili kudumisha amani, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaendelea na juhudi za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wao, viongozi wa makundi ya Sungusungu kutoka mikoa mbalimbali waliishukuru Serikali kwa kutambua mchango wao, huku wakiahidi kuendeleza mshikamano na nidhamu katika kutekeleza majukumu yao.
Hafla hiyo imehudhuriwa pia na viongozi wa kitaifa, wakuu wa mikoa husika, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wananchi waliojitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Ziara ya Rais Samia mkoani Mwanza inaendelea, ambapo anatarajiwa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi katika maeneo mengine ya jiji hilo.
No comments:
Post a Comment