Tuesday, November 01, 2016

WADAU WA HABARI WALIVYOSHIRIKI KUTOA MAONI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA ZA HABARI


Jovina Bujulu.

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inatarajia kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari. Muswada huu utatoa mwelekeo na dira ya tasnia ya Habari katika utendaji kazi wake.

Kabla ya kuwasilisha muswada huu Bungeni Serikali ilipokea maoni kutoka kwa wadau wa habari, vyama visivyokuwa vya Kiserikali (NGO’s) na taasisi mbali mbali kuhusu namna na jinsi wanavyotaka muswada wa habari uwe mwongozo wa tasnia ya habari.Miongoni mwa wadau ambao walifikisha maoni Serikalini ni pamoja na Baraza la Habari Tanzania ( MCT), Tanzania Citizens Information Bureau (TCIB), Tanganyika Law Society, Sikika pamoja na Nation Organization for Legal Assistance (NOLA).

Wadau wengine ni Jukwaa la Wahariri (TEF), Kituo cha Haki za Binadamu (LHCR), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Tanzania Human Rights Defenders (THRDs), Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) na Taasisi ya Wanahabari Nchi za Kusini Mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN). 

Baadhi ya mambo yaliyowasilishwa Serikalini na wadau hao mnamo Machi, 31, 2016 ni pamoja na kuimarisha utendaji wa vyombo vya habari nchini, kuendeleza weledi katika taaluma ya habari na kulinda usalama wa wanahabari.

Mapendekezo yao kwa kiasi kikubwa ndiyo yaliyopo katika muswada wa sheria inayopendekezwa ambao umewasilishwa ili ujadiliwe katika kamati ya Bunge na Huduma za Jamii. Kamati hii na wadau inakutana mjini Dodoma kwa sasa.Baadhi ya mambo yaliyomo katika muswada huu ni pamoja na kuunda Bodi ya Ithibati, ambayo itatoa ithibati na vitambulisho kwa wanahabari,kusimamia kanunu za maadili ya wanahabari na kuishauri Serikali katika suala la elimu na mafunzo kwa wanahabari.

Kwa kuangalia baadhi ya maoni yaliyopendekezwa na wadau, na masuala yaliyomo katika muswada huu wa sheria inayopendekezwa, yote yameegemea katika kuipa tasnia hadhi kwa kuzingatia vigezo vya weledi, maadili na elimu kwa wanahabari.Aidha, wadau waliwasilisha kuwa uwepo uhuru wa vyombo vya habari na kwamba wanahabari wawe huru kutafuta, kuchunguza na kuchapisha habari bila kuingiliwa. 

Suala hili lipo katika muswada wa sheria inayopendekezwa na kwamba hakuna mwandishi ayekatazwa kutafuta na kuchapisha habari ila muswada lakini uhuru huo sio kigezo cha kuingilia sheria nyingine.Wadau hao pia walipendekeza sheria ijayo itoe fursa kwa Serikali kuendelea kusajili vyombo vya habari bila kuweka masharti , jambo ambalo lipo pia katika sheria inayopendekezwa kwamba Serikali itaendelea kusajili kwa kuzingatia kanunu, sheria na taratibu zilizopo.

Kuhusu suala la ulinzi na usalama wa waandishi , wadau walipendekeza kuwa wamiliki wa vyombo vya habari wawe na wajibu wa kuzingatia usalama wa wanahabari wanapokuwa kazini ,suala ambalo limo katika muswada wa sheria inayopendekezwa ambapo inamtaka kila mwajiri kuweka Bima na hifadhi ya jamii kwa kila mtu aliyeajiriwa katika chombo cha habari husika.

Kutokana na tasnia ya habari kukosa taasisi inayosimamia wanahabari na vyombo vya habari, muswada wa sheria hii umekuja wakati muafaka kwani endapo itapitishwa itakuwa mkombozi wa wanahabari na tasnia yenyewe. Aidha sheria hii itawapa wanahabari mwelekeo wa kazi na kujua ni mahali gani wanakosea na jinsi ya kujisahihisha. Hii ni kutokana na kuwepo kwa Baraza Huru la Habari ambalo litaandaa na kuidhinisha kanuni za maadili ya wanahabari.

Kwa wadau wa habari, ambao kwa muda mrefu wamekuwa na kiu ya kupata chombo ambacho kitaelekeza na kuongoza tasnia hii, huu ni wakati muafaka kwao kuiunga mkono muswada wa sheria hii ili upitishwe kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.Tumeona manufaa mengi ya elimu na weledi kwa wanahabari,kwa kuwepo kwa mfuko wa mafunzo ya habari, usalama wao kwa kuwataka waajiri wao kuwawekea bima. Kwa kupitisha sheria hii wanahabari watatekeleza wajibu wao kwa weledi na ufanisi zaidi.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...