Tuesday, November 08, 2016

BUNGE LAISHAURI SERIKALI KUTOSAINI EPA

index

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.
Mkutano wa Tano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeishauri Serikali kutosaini Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi Kati ya Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU) – (EPA) kwa kuwa hauna manufaa kwa nchi ya Tanzania.
Ushauri huo umetolewa leo mjini Dodoma na wabunge wa Bunge hilo baada ya kuujadili mkataba huo kwa kina kwa kutoa maoni yao ambapo wengi wameunga mkono kutosainiwa kwa mkataba huo.
Baadhi ya wabunge waliopata nafasi ya kutoa maoni yao katika mjadala huo ni Mbunge wa Mtwara Vijijini(CCM) Mhe. Hawa Ghasia amemshauri Mhe. Rais Dkt .John Pombe Magufuli kutosaini mkataba huo kwa kuwa mkataba huo una hasara nyingi kwa taifa kuliko faida.
”Kwa kuzingatia mkataba umeruhusu uingizaji na utoaji wa bidhaa huru na ukizingatia hakuna nchi hata moja ya Ulaya ambayo Tanzania inapeleka bidhaa zake hivyo mkataba huu hauna maslahi kwa watanzania”, alisema Mhe. Ghasia.
Ameongeza kuwa Tanzania sio nchi ya kwanza kutosaini mkataba huo kwani kuna nchi kama Angola, Nigeria, na Gambia hazijasaini,ameongeza kuwa kama Tanzania itakubaliana na mkataba huo utaua viwanda pamoja na biashara za Tanzania.
Kwa upande wake Mbunge wa Nzega Mjini Hussein Bashe amesema kuwa tatizo lililopo katika mkataba huo ni kutoitambua nchi kama nchi na badala yake kuangalia nchi zote kwa pamoja hivyo amewashauri wabunge kuhoji kuanzia kwenye kiini cha tatizo.
“Kwa kuwa kifungu cha 143 cha mkataba huo kinaruhusu kupeleka marekebisho, naishauri Serikali yetu ipeleke marekebisho ya kupendekeza kila nchi iingie mkataba kivyake kulingana na maslahi ya nchi yake”, alisema Bashe.
Aidha, Mbunge wa Mwibara (CCM) Mhe.Kangi Lugola amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kukataa kusaini mkataba huo kwani ni miongoni mwa mikataba mibovu kati ya mikataba iliyowahi kuletwa nchini kutoka katika nchi za Ulaya.
“Kama tukikubali kusaini mkataba huu nchi hii itakuwa dampo la bidhaa mbalimbali za ajabu kutoka nje na hivyo kupelekea kushindwa kutimiza dhamira ya nchi ya kuimarisha viwanda vyetu”, alisema Mhe. Lugola.
Naye, Mbunge wa Mchinga (CUF) Mhe. Hamidu Bobali amesema kuwa mkataba huo haufai kwa maslahi mapana ya taifa hili kwani unataka kuondoa ushuru kwa bidhaa zinazoingia nchini wakati nchi ya Tanzania inaingiza bidhaa nyingi kutoka nje kuliko kupeleka bidhaa nje ya nchi.
“Kama tukikubali tukaondoa ushuru wa kuingiza bidhaa kutoka nje basi tutapoteza mapato mengi yanayotokana na kuwepo kwa bandari pia tunatakiwa tujiulize kama mkataba umeruhusu uingizaji na utoaji wa bidhaa huru je nchi yetu ina bidhaa zinazokidhi vigezo vya kuingia katika nchi za Ulaya?” , alihoji Mhe. Bobali.
Mhe. Bobali ametoa rai kwa Serikali kuileta Bungeni mikataba mikubwa kama ya gesi na madini kwa ajili ya kujadiliwa kwa kina ili kuepuka kusaini mikataba isiyo na tija kwa Taifa.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...