Monday, May 12, 2014

Soma Taarifa Ya Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT Tanzania) Kuhusu Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika taarifa yake ya mwaka 2012/2013

1. Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT Tanzania) kimesononeshwa sana na hoja za ukaguzi zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika taarifa yake ya mwaka 2012/2013. Taarifa ya CAG inaonyesha kuwa fedha za umma katika mwaka wa fedha uliotajwa zilitumiwa vibaya na watu waliokabidhiwa mamlaka ya kuzitunza na kuzitumia kwa ajili ya wananchi. 
Taarifa inaonyesha, kwa mfano, kwamba fedha za walipa kodi shilingi bilioni 1.6 ziliibwa kwa kulipa watumishi hewa waliokwishafariki dunia. Aidha, taarifa hiyo inaonyesha kuwa magari 11 ya Wizara ya Viwanda na Biashara yalitoweka katika mazingira tatanishi na hadi leo hayajulikani yalipo. Kwa kifupi, magari haya yamekwepuliwa na wajanja. 

2. Fedha hizi zimefujwa katika nchi ambayo zaidi ya theluthi ya watu wake wanaishi katika ufukara wa kutupwa, elimu inayozidi kuporomoka mwaka hadi mwaka, watu wanaopeteza maisha yao kwa magonjwa yanayotibika kutokana na huduma mbaya sana za afya, zaidi ya asilimia 90 hawana hifadhi ya jamii, zaidi ya nusu ya wananchi hawana maji safi na salama na miundombinu inayosombwa na maji kila mvua zikinyesha. Kwa hakika inatia hasira kuona matumizi ya hovyo ya fedha za walipa kodi tena bila hatua stahiki kuchukuliwa na watu waliokabidhiwa mamlaka na wananchi haohao wanaoteseka na wanaowaibia. 

3. Aidha, ACT Tanzania inachukizwa kuona kuwa maendeleo ya nchi yanachangiwa na wafanyabiashara wadogo, wafanyakazi na wafadhili ilhali wafanyabiashara wakubwa na wawekezaji wanapata ruzuku na serikali kupitia misamaha ya kodi yenye thamani ya shilingi 1.5 trilioni. 

4. ACT-Tanzania imekokotoa hoja za ukaguzi na kukuta kwamba kwenye masuala ya Serikali kuu pekee thamani ya hoja ni shilingi bilioni 867 ikiwa ni fedha zilizopotea. Kiwango hiki cha fedha kingeweza kumaliza ukarabati wa bandari ya Dar Es salaam kwa kujenga gati mpya, au kuweza kujenga vyuo vya ufundi vya VETA katika kila wilaya nchini. 

5. ACT-Tanzania imekaribisha kwa mikono miwili taarifa ya kwanza ya ukaguzi wa vyama vya siasa nchini. Hii ni historia ya kuenzi katika ujenzi wa jamii ya uwajibikaji. ACT-Tanzania inatoa rai kwa CAG kuweka wazi mahesabu ya kila chama ili wanachama wa vyama hivyo wajue namna vyama vyao vinavyoendeshwa. Vilevile ACT-Tanzania inamtaka CAG atoe Maelezo ya kina ni Kwanini hajakagua hesabu za chama cha CCM, lini atakagua na lini ataweka wazi mahesabu yao. 

6. ACT Tanzania imesikitishwa na Taarifa ya awali ya CAG inayoonyesha kuwa hakuna hata chama kimoja cha siasa kilichowasilisha mahesabu yake ambacho kilifuata taratibu za kiuhasibu katika kuwasilisha taarifa yake, jambo ambalo linatia shaka juu ya mwenendo wa matumizi ya fedha za umma katika vyama hivyo. 

7. ACT Tanzania inawaomba wananchi waitafakari taarifa ya CAG na kujitathimini na kuchukua hatua stahiki kuipumzisha CCM katika chaguzi zijazo kwa kuwa serikali yake imethibitisha miaka nenda rudi kuwa haiwezi kutunza na/au kutumia fedha za umma kwa maendeleo ya nchi na wananchi wake. 

8. ACT-Tanzania inawahimiza wabunge wenye kuamini katika sera za mrengo wa kushoto na dhana ya uwajibikaji kutumia taarifa ya CAG kwa kina wakati wa mijadala ya Bajeti, na kukataa kupitisha Bajeti za wizara ambazo CAG ameainisha madudu. 

Pamoja na Salamu za ACT Tanzania. 
(Signed) 
Samson Mwigamba 
Katibu Mkuu ACT-Tanzania

* ACT Tanzania ni Chama cha Siasa kilichoundwa kwa kufuata misingi ya Demokrasia Jamii na chenye shabaha kuu ya kusimamia Mabadiliko na Uwazi.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...