Friday, January 03, 2014

WANAKWAYA ARUSHA WALIPULIWA KWA BOMU

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas.
WANAKWAYA sita wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Kalory Rwanga, Usa River, mkoani hapa, wamelazwa katika Hospitali ya Misheni na ya Tengeru, Arumeru baada ya kujeruhiwa kwa bomu.
Walikutwa na masahibu hayo juzi muda mfupi baada ya kutoka kanisani kwenye Mkesha wa Mwaka Mpya saa 6.30 usiku, meta 100 kutoka Kanisa hilo, eneo la Kisangani.
Mganga Msaidizi wa hospitali hiyo, iliyoko chini ya Kanisa Katoliki, Fredrick Mathew, alithibitisha jana kupokewa majeruhi watano, huku wawili wakiwa na hali mbaya na wengine wakiendelea vizuri.
Alitaja majeruhi hao kuwa ni Theresia Lesitare (33), Philipo Ambrose (22), Alphonce Nyigo (19), Mary Merikiory (40) na Anna Mathew (19) wote wakazi wa Lake Tatu, Usa River.
Majeruhi mwingine ambaye hali yake si nzuri, Annet Baltazar (16) amelazwa katika Hospitali ya Tengeru. Alisema majeruhi hao waliumia miguuni kwa kuchanwa na mlipuko huo na baadhi ya vipande vya bomu, vilitolewa kwenye miili yao na baadhi yao kushonwa kwa nyuzi kadhaa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kupata taarifa za tukio hilo na kueleza, kwamba uchunguzi wa tukio umeanza mara moja na atatoa taarifa ukikamilika.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, Merikiory, alisema baada ya kutoka kanisani akiwa na wanakwaya wenzake, waliondoka kuelekea nyumbani, Lake Tatu.
Alisema wakiwa barabarani, waliona gari aina ya Toyota Land Cruiser likienda kwa kasi na lilipowakaribia, walisikia mlipuko na wakajikuta wamelala kando ya barabara huku baadhi yao wakivuja damu miguuni na tumboni.
Aliongeza kuwa gari hilo, halikusimama na lilipofika mbele waliokuwamo walifyatua mabomu ya kutoa machozi, kutawanya makundi ya watu mbalimbali waliokuwa wakionekana barabarani.
Alisema waliomba msaada kwa Paroko wa Kanisa hilo, Patrick Njau, ambaye alitoa gari na kuwapeleka Hospitali ya Misheni na wengine wakipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Tengeru kwa matibabu zaidi.
Askofu alia
Akizungumza huku akitokwa machozi baada ya kutembelea majeruhi, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Josephat Lebulu alisema ameshangazwa na tukio hilo. Alisisitiza kuwa Kanisa Katoliki, limechoka kuandamwa na matukio ya aina hiyo.
“Waumini wanakosa gani hadi watupiwe bomu, kwa nini polisi wako kimya hadi leo wasiseme? Kuna siri gani? Kwa nini kila siku ni Wakatoliki tu ndio wanapigwa mabomu, tunataka haki itendeke, watu wametoka kanisani usiku, wamekosa nini? Usalama uko wapi?” Alihoji.
Aliendelea: “Tumekosa nini, kupigwa mabomu kila siku hapa Arusha? Tumeshuhudia Olasiti, tukashuhudia Soweto sasa ni hapa Usa,” alisema. “Na kwa hili Kanisa hatutakubali hata kidogo, tunataka wahusika wawajibishwe na walioficha uovu huu wawajibishwe la sivyo viongozi walioficha uovu huu wawajibishwe, Mungu atasimama kwa ajili yetu,” alisema.
Mei mwaka jana, bomu lililorushwa liliua watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 60 kwenye Kanisa
Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Parokia ya Olasiti, mjini Arusha.
Waumini walikuwa wamejumuika katika misa ya uzinduzi wa Kanisa hilo. Misa hiyo ilikuwa ikiongozwa na Balozi wa Vatican nchini na Mwakilishi wa Papa Francis, Askofu Francisco Padila kwa kushirikiana na Askofu Lebulu.
Taharuki Dar
Katika hatua nyingine, hali ya taharuki ilizuka jana maeneo ya Shekilango, Dar es Salaam baada ya kudaiwa kuwapo bomu la kurushwa kwa mkono kwenye eneo la njia ya waenda kwa miguu, karibu na eneo la ujenzi wa barabara ya Morogoro.
Gari la Polisi kutoka Kituo kidogo cha Urafiki, lilifika eneo hilo saa 4 asubuhi na kuzungushia mkanda wa hadhari eneo lililodaiwa kuwapo bomu.
Walifanya hivyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa mpita njia, aliyeona kitu hicho kilichoelezwa kuwa ni bomu, ingawa baadaye taarifa ya Polisi ilisema halikuwa bomu.
Gazeti hili lilifika eneo la tukio na kushuhudia, ambapo polisi walilazimika kufukuza mamia ya watu waliokuwa wakimiminika kuliangalia, jambo ambalo ilikuwa hatari.
Alpha Sidadi (29) ambaye alikuwa wa kwanza kuona kifaa hicho, alisema ndiye aliwasiliana na polisi kuwaeleza juu ya kitu hicho.
Kwa mujibu wa Sidadi, alimsubiri mama yake, Asha Sidadi aliyekuwa akitoka Kinondoni na kumweleza kuwa waliwasiliana na polisi wanayefahamiana naye, aliyewasiliana na wenzake na kufika eneo la tukio.
Mama huyo alisema alipofika na kuelezwa na mwanawe na kuona kitu hicho kikiwa kama nanasi jeusi na aliwasiliana na polisi ambao walifika mara moja na kusema wanasubiri wataalamu wa kutegua mabomu.
Mmoja wa Polisi aliyefika eneo hilo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alikiri kitu hicho kufanana na bomu la kutupa kwa mkono. Alisema walikuwa wakisubiri wataalamu wathibitishe na akataka wananchi kuacha kukimbilia katika maeneo ya hatari kwa nia ya kutaka kushuhudia.
Juma Maulid ,mfanyabiashara wa maeneo hayo alidai waliwahi kukuta kifaa kama hicho katika eneo hilo.
Akizungumzia kuhusu suala hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema tofauti na ilivyodhaniwa na watu wengi, kitu hicho hakikuwa bomu, isipokuwa ni mwanasesere mwenye umbo mfano wa bomu.
“Hata hivi sasa ninavyokueleza kipo hapa ofisini kwangu. Unajua siku hizi kuna vitu vinatengenezwa kwa mifano, mfano unaweza kukuta chupa za manukato zenye mfano wa bomu au wanasesere wa kuchezea watoto wenye mfano huo, ukweli kitu kile hakikuwa bomu kama ilivyodhaniwa,” alisema Wambura.
Alisema vitu vingi siku hizi vikiwamo vifaa vya kuchezea watoto, vimetengenezwa kwa maumbo mbalimbali.
CHANZO: HABARI LEO

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...