Dar es Salaam.Wafuasi wa Chadema wanaomuunga mkono aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe na wanaounga mkono uongozi wa juu, jana walitwangana tena muda mfupi baada ya kuondoka eneo la Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Tukio hilo limetokea huku Mahakama hiyo ikiahirisha hadi leo, kutoa uamuzi wa maombi ya Zitto kuzuia kujadiliwa na Kamati Kuu ya Chadema.
Katika maombi hayo namba 1 ya mwaka 2014, Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, anaiomba Mahakama iizuie Kamati Kuu ya Chadema kumjadili na au kuchukua uamuzi wowote kuhusu uanachama wake hadi kesi yake ya msingi aliyoifungua mahakamani hapo itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Uamuzi wa maombi hayo ulipangwa kutolewa jana na Jaji John Utamwa ambaye hata hivyo, alisema alikuwa hajamaliza kuandika uamuzi huo na kuahirisha shauri hilo hadi leo mchana.
Maombi hayo ya Zitto ya zuio la muda la kujadiliwa na kuchukuliwa uamuzi wowote kuhusu uanachama wake yametokana na kesi ya msingi aliyoifungua mahakamani hapo Januari 2, 2014, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Katika kesi hiyo, Zitto pia anaiomba Mahakama Kuu imwamuru Katibu Mkuu wa Chadema ampatie mwenendo na taarifa za kikao cha Kamati Kuu za kumvua nyadhifa zake zote alizokuwa nazo ndani ya chama na iwazuie walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake ya ubunge wa Kigoma Kaskazini.
Mapigano
Baada ya kuahirishwa kwa shauri hilo, wanachama wa makundi yote waliondoka eneo la Mahakama wakiendelea kuimba na kushangilia lakini walipofika eneo la Mahakama ya Rufani ghafla walianza kupigana ngumi na mawe. Baadhi yao walikamatwa na askari kutokana na vurugu hizo.
Awali, wafuasi hao walifika mapema asubuhi katika viwanja vya Mahakama tayari kusikiliza uamuzi huo.
Ulinzi ulikuwa umeimarishwa na askari polisi wakiwamo wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), waliokuwa na silaha pamoja na mabomu ya machozi walikuwa wametanda.
Pia kulikuwa na askari wa Kikosi cha Mbwa pamoja na gari la maji ya kuwasha.
Licha ya kuwahi, ni wafuasi wachache walioruhusiwa kuingia ndani ya u`kumbi wa Mahakama tena baada ya kuandikisha majina yao huku wakitambuliwa na viongozi wao waliokuwapo.
No comments:
Post a Comment