Wednesday, August 20, 2008

Rais Mwanawasa afariki kweli


RAIS wa Zambia Levy Mwanawasa (59), amefariki dunia nchini Ufaransa ambako amekuwa akipatiwa matibabu baada ya kupata mstuko.
Kifo cha Mwanawasa ambaye ni kipenzi cha nchi za Magharibi kutokana na msimamo wake katika mapambano dhidi ya ufisadi, kimetokea miezi takriban miwili baada ya kuzushiwa kifo.
Makamu wa Rais wa Zambia, Rupia Banda, amenukuliwa na Shirika la Habari la Uingereza (Reuters) akithibitisha kutokea kwa kifo cha Rais Mwanawasa.
Banda alifafanua kwamba kutokana na kifo hicho cha Rais Mwanawasa, nchi itakuwa katika maombelezo ya siku saba za msiba huo mzito.
Mwanawasa pia atakumbukwa kutokana na msimamo wake wa kuwa mmoja wa viongozi wa Afrika wanaomkosoa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, kutokana na matendo yake ya ukiukaji demokrasia na utawala bora.
"Ndugu zangu wananchi, kwa majonzi na masikitiko makubwa napenda kuarifu watu wa Zambia kwamba, Rais wetu Dk Levy Patrick Mwanawasa, amefariki leo asubuhi (jana)," alisema Makamu wa Rais Banda kupitia televisheni ya taifa ya nchi hiyo na kuongeza:
"Pia ningependa kuarifu kwamba, maombelezo ya kitaifa ya kifo cha Rais yatafanyika kwa muda wa siku saba."
Kwa mujibu wa Katiba ya Zambia, Banda ndiye ambaye anatarajiwa kukaimu madaraka hayo ya Rais hadi utakapoitishwa uchaguzi.
Mwanawasa aliweza kujijengea heshima miongoni mwa Wazambia, baada ya kuwezesha utajiri wa madini ya shaba kunufaisha raia wake wengi.
Pia anaheshimiwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na nchi fadhili za Magharibi, ambazo ziliamua kuongeza msaada wa mabilioni ya dola kwa nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika.
Uamuzi wa IMF na nchi fadhili za Magharibi kuongeza msaada kwa Zambia, unatokana na juhudi nzito za Mwanawasa katika kuendesha kampeni nzito dhidi ya ufisadi, ikiwa ni za kwanza tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1964 kutoka kwa Waingereza.
Miongoni mwa watu waliokumbwa na operesheni hiyo ya ufisadi, ni Rais aliyemrithi Frederick Chiluba.
Hivi karibuni, baada ya kutokea hali ya tete ya nchini Zimbawe baada ya kuvurugika kwa duru ya kwanza ya uchaguzi, Mwanawasa alimshutumu Mugabe akisema anataka kuleta balaa jingine la machafuko barani Afrika.

Historia fupi ya Mwawasa

Mwanawasa alizaliwa Mufurira, eneo la Ukanda wa Shaba, Septemba 3,1948 na kuanza kuibuka katika siasa wakati akiwa Makamu wa Rais wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zambia, ambacho kilifanya maandamano kadhaa kuunga mkono harakati za ukombozi wa nchi ya Afrika Kusini.
Baada ya kuhitimu chuo mwaka 1973, taratibu Mwanawasa alianza kujiimarisha kama mwanasheria anayeshimika katika kipindi cha miaka 20 iliyofuata.
Katika moja ya kesi maarufu, alifanikiwa kumtetea makamu wa zamani wa rais, Christon Tembo na wenzake walioshtakiwa kwa makosa ya uhaini mwaka 1989, akiwa amewaokoa katika hukumu ya kifo kama wangepatikana na hatia.
Akiwa mmoja wa waasisi wa chama cha Movement for Multi- Party Democracy (MMD), Mwanawasa alimsaidia Frederick Chiluba kumshinda Rais Kenneth Kaunda katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini Zambia mwaka 1991.
Mwishoni mwa miaka ya 1991 aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Zambia, lakini akajiuzulu miaka mitatu baadaye kutokana na kushindwa kuvumilia matumizi mabaya ya ofisi na rushwa iliyokuwa imekithiri wakati wa utawala wa Chiluba.
Wakati akiendelea kuwa mwanachama wa MMD, Mwanawasa aliendelea na shughuli zake kwenye jumuiya ya wanasheria hadi mwaka 2001.
Mwanawasa alinusurika katika ajali ya gari Desemba mwaka 1991 na akalazwa hospitalini kwa miezi mitatu. Ajali hiyo mbaya ilimfanya atembee kwa kuchechemea na kuzungumza kwa shida.
Baada ya kuitwa kurejea MMD kwa kutumia vikao vya pembeni na Chiluba, Mwanawasa aligombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2001.
Kwa mshangao wa kila mtu, Mwanawasa alikorofishana na Chiluba mara baada ya kuapishwa na akaanza kampeni ya kusafisha rushwa, kampeni ambayo ilidaiwa kuwa ya kutafuta mchawi dhidi ya serikali ya zamani.
Mwezi Aprili, 2006, Mwanawasa alikumbwa na kiharusi, lakini akapona mapema baada ya kutibiwa nchini Uingereza.
Miezi mitatu baadaye, alimshinda mpinzani wake wa kisiasa Michael Sata na kurejea madarakani kwa kipindi cha pili, akiwa ameshinda kwa kura chache.
Tofauti na aliyemtangulia, Mwanawasa alipata mafanikio makubwa katika maendeleo. Chini ya utawala wa Mwanawasa, Zambia imekuwa na maendeleo makubwa ya kiuchumi, huku wawekezaji wa nje wakiwekeza mabilioni ya fedha.
Mwanawasa alikuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika mwaka 2007 na alisifiwa kwa juhudi zake zisizo na kikomo katika kujaribu kumaliza mgogoro wa kisiasa ulioibuka nchiniZimbabwe baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Machi 2008.
Mwanawasa ameacha mke Maureen Luchendo Mwanawasa na watoto sita.
- Reuters

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...