Wednesday, May 28, 2025

WAZIRI MKUU MAJALIWA AKUTANA NA VIONGOZI WA WIZARA YA ARDHI YA JAPAN NA SHIRIKISHO LA WAWEKEZAJI (JAIDA)





Tokyo, Japan – Mei 27, 2025

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafirishaji na Utalii wa Japan, Mheshimiwa Hiromasa Nakano, katika Makao Makuu ya Wizara hiyo jijini Tokyo, Japan.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Japan hususan katika maeneo ya ardhi, miundombinu na usafirishaji. Viongozi hao walijadili njia za kuendeleza miradi ya kimkakati inayolenga kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Katika hatua nyingine ya ziara hiyo, Mheshimiwa Majaliwa alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Rais wa Shirikisho la Wawekezaji katika Sekta ya Miundombinu la Japan (Japan Infrastructure Development Association – JAIDA), Bw. Miyamoto Yoichi, pamoja na ujumbe wake.

Mazungumzo hayo yalijikita katika kuhamasisha wawekezaji wa Japan kuwekeza Tanzania, hususan katika sekta za ardhi, miundombinu na usafirishaji. Waziri Mkuu aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji, ikiwa ni pamoja na sera thabiti, usalama wa mitaji, na fursa lukuki zinazopatikana kupitia programu na miradi ya kimkakati ya serikali.

Mheshimiwa Majaliwa alisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania iko tayari kushirikiana na wawekezaji kutoka Japan katika kuendeleza miradi ya kielelezo yenye lengo la kuchochea maendeleo ya taifa, na kutoa ajira kwa Watanzania.

Kwa upande wao, viongozi wa JAIDA walionesha nia ya dhati ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuwekeza kwenye miradi yenye tija, huku wakivutiwa na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kukuza uchumi wa nchi.

Mwisho wa ziara hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa aliwashukuru viongozi wa Serikali ya Japan na wadau wa sekta binafsi kwa ushirikiano wao na kuahidi kuendeleza mazungumzo hayo kwa ajili ya manufaa ya pande zote mbili.

No comments:

MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO ATEMBELEA KAMPUNI YA KIMATAIFA YA VIFAA TIBA NCHINI ITALIA

ROMA, ITALIA – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, ametembelea kampuni ya kimataifa ya uzalis...