Dodoma, 8 Mei 2025 — Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu mpya wa FP-ICGLR, Dkt. Deo Mwapinga, katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Spika Dkt. Tulia alimpongeza Dkt. Mwapinga kwa kuchaguliwa kushika nafasi hiyo ya juu ya kikanda na kumhakikishia kuwa Bunge la Tanzania litaendelea kushirikiana naye kikamilifu katika kuimarisha ushirikiano wa mabunge ya nchi wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu.
Aidha, Spika alieleza kuwa Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika masuala ya demokrasia, utawala bora, na maendeleo ya pamoja kupitia taasisi za kikanda kama FP-ICGLR.
Kwa upande wake, Dkt. Mwapinga, ambaye alichaguliwa tarehe 25 Aprili 2025 jijini Luanda, Angola, ameahidi kutumia nafasi hiyo kwa kulijenga jukwaa hilo kuwa na sauti thabiti na inayojali maslahi ya wananchi wa ukanda huu, kwa kuzingatia misingi ya haki, amani na ushirikiano wa mabunge.
Dkt. Mwapinga ataongoza FP-ICGLR kwa kipindi cha miaka mitatu, kwa mujibu wa katiba ya Jukwaa hilo, huku akiwa na nafasi ya kurejewa kwa mujibu wa taratibu.
FP-ICGLR (Forum of Parliaments of the International Conference on the Great Lakes Region) ni jukwaa linalojumuisha mabunge ya nchi wanachama wa ICGLR likiwa na dhamira ya kuimarisha amani, usalama, haki na maendeleo katika Ukanda wa Maziwa Makuu kupitia mchango wa mabunge.
#FPICGLR #BungeTanzania #TuliaAckson #UshirikianoWaKikanda #DiplomasiaYaBunge
No comments:
Post a Comment