Serikali kupitia taasisi zake mbalimbali imeanza kuchukua hatua za haraka na za kimkakati kukabiliana na changamoto kubwa ya magugu maji katika Ziwa Victoria, ambayo kwa muda mrefu yameathiri shughuli za kiuchumi, kijamii na kimazingira katika maeneo yanayozunguka ziwa hilo.
Katika jitihada hizo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Cyprian Luhemeja, hivi karibuni alifanya ziara ya kikazi katika mkoa wa Mwanza kushuhudia hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na hali hiyo. Akiwa ziwani, Mhe. Luhemeja aliangalia kwa karibu zoezi la ukataji na uondoshaji wa magugu maji, zoezi linalofanyika kwa ushirikiano kati ya serikali za mitaa, Wizara ya Maji, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Bodi ya Bonde la Ziwa Victoria, na taasisi nyingine zinazohusika na usimamizi wa mazingira.
Takwimu zinaonesha kuwa hadi kufikia Mei 10, 2025, zaidi ya tani 600 za magugu maji zimeondolewa kutoka katika maeneo mbalimbali ya Ziwa Victoria, ikiwa ni ishara ya utekelezaji mzuri wa awamu ya kwanza ya operesheni hiyo ya kitaifa.
Mhe. Luhemeja alisema kuwa magugu maji, hasa yale ya zamani ambayo yameota kwa muda mrefu, yanahitaji nguvu na teknolojia ya kisasa ili kuondolewa kikamilifu. “Changamoto hii si ya kuiachia taasisi moja, bali ni jukumu letu sote kama wadau wa mazingira. Serikali imeanza kuchukua hatua za haraka, lakini tunahitaji ushirikiano kutoka kwa wananchi, taasisi binafsi na washirika wa maendeleo,” alisema.
Hatua mbili kuu zimebainishwa katika kukabiliana na changamoto hiyo:
-
Kupunguza kasi ya ukuaji wa magugu maji kwa kutumia njia za muda mfupi kama ukataji wa mikono na mashine, ili kuruhusu shughuli za kijamii na kiuchumi kama uvuvi na usafirishaji kuendelea.
-
Ununuzi wa mashine za kisasa za kukata magugu maji, ambazo zitatumika kusafisha maeneo yaliyovamiwa kwa kiasi kikubwa. Manunuzi haya yanatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mwezi mmoja hadi mmoja na nusu ujao.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, serikali imesisitiza kuwa kazi bado ipo mbele, hasa kwa kuzingatia ukubwa wa eneo la Ziwa Victoria na kasi kubwa ya uotaji wa magugu hayo. Viongozi wa mikoa na wataalamu wa mazingira wametakiwa kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha hali hiyo inadhibitiwa kwa wakati.
Aidha, serikali imetoa wito kwa wadau wote, wakiwemo wazalishaji wa chakula cha samaki, wafugaji wa samaki, na wananchi wa maeneo ya mwambao, kuhakikisha wanazingatia matumizi sahihi ya rasilimali za maji ili kusaidia jitihada za uhifadhi wa mazingira na usalama wa ikolojia ya ziwa hilo.
“Hatua hizi tunazochukua leo ni msingi wa kuimarisha mustakabali wa Ziwa Victoria. Mazingira salama ni msingi wa uchumi wa buluu, afya ya wananchi wetu na kizazi kijacho,” alisema Mhe. Luhemeja.
No comments:
Post a Comment