Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeandika historia mpya kwa kuibuka kidedea kama Mkandarasi Bora wa Kibiashara wa Mwaka 2025 katika Tuzo za Tanzania Real Estate Awards (TREA), tukio la kifahari lililoandaliwa na kampuni ya Corporate Solution Worldwide (CSW Tanzania).
Tuzo hiyo ni ushahidi wa wazi wa viwango vya juu vya ubora, ufanisi na umahiri wa kitaalamu vinavyoonyeshwa na NHC katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi kote nchini, hasa katika sekta ya makazi na maendeleo ya miji.
Tukio hilo la utoaji wa tuzo lilifanyika jijini Dar es Salaam likiwakutanisha wadau wakuu wa sekta ya ardhi, makazi, ujenzi, wawekezaji wa ndani na nje ya nchi pamoja na taasisi binafsi na za umma zinazojihusisha na maendeleo ya sekta hiyo muhimu.
Jumla ya tuzo 10 zilitolewa, kila moja ikiwakilisha kipengele muhimu katika sekta ya ardhi na ujenzi—ikiwemo:
-
Mradi Bora wa Makazi,
-
Ubunifu wa Majengo,
-
Mwekezaji Bora,
-
Kampuni Bora ya Uendelezaji Miliki,
-
Mkandarasi Bora wa Makazi,
-
na Mkandarasi Bora wa Kibiashara—ambapo NHC ilitwaa ushindi huo mkubwa.
Tuzo ya NHC ilipokelewa kwa heshima na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Miliki wa Shirika, Bw. Elias Msese, na kukabidhiwa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi, Stephano Kyando, aliyemwakilisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi.
Katika hotuba yake ya kupokea tuzo, Bw. Msese alisema:
“Tuzo hii ni matokeo ya kazi ya pamoja, ubunifu na ufuatiliaji wa karibu wa miradi yetu. Inaonyesha jinsi ambavyo Shirika la Nyumba la Taifa linavyoweka mbele masuala ya ubora na ufanisi katika kila hatua ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi.”
NHC imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza miradi ya kimkakati kama vile:
-
Samia Housing Scheme – Kawe,
-
Morocco Square,
-
711 Kawe ,
-
na mingineyo inayolenga kutoa makazi bora, ya kisasa na yenye mazingira rafiki kwa jamii ya Kitanzania.
Kupitia ushindi huu, NHC imejidhihirisha tena kama chombo madhubuti katika kutimiza ndoto ya Serikali ya Awamu ya Sita ya makazi bora kwa kila Mtanzania, sambamba na ajenda ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Tuzo ya TREA inalenga kuhamasisha ushindani chanya, uadilifu, na ubunifu miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika ujenzi wa taifa kupitia sekta ya ardhi na makazi. Kwa NHC, ushindi huu si mwisho, bali ni kichocheo cha kuongeza kasi ya utoaji huduma bora zaidi kwa wananchi.
Shirika la Nyumba la Taifa linatoa shukrani kwa CSW Tanzania na waandaaji wa TREA kwa kutambua juhudi hizi. Tunaahidi kuendelea kuongoza kwa ubora na kuleta mageuzi chanya katika sekta ya ujenzi na makazi.
No comments:
Post a Comment