Tuesday, May 20, 2025

RAIS WA TANZANIA MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN AMPOKEA RAIS WA NAMIBIA MHE. NETUMBO NANDI-NDAITWAH IKULU, DAR ES SALAAM






Dar es Salaam, 20 Mei 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amempokea rasmi mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mheshimiwa Netumbo Nandi-Ndaitwah, mara baada ya kuwasili katika viunga vya Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kitaifa.

Ziara hii ni ya kihistoria na ya kwanza kufanywa na Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah tangu alipochaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Namibia. Kupokelewa kwake Ikulu kulihusisha gwaride rasmi la heshima pamoja na kupigwa kwa nyimbo za taifa za nchi zote mbili kuashiria urafiki, mshikamano na ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Namibia.

Katika mazungumzo yao, viongozi hao wawili wanatarajiwa kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kimaendeleo, kiuchumi, kijamii na kisiasa baina ya nchi hizi mbili rafiki. Miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kupewa kipaumbele ni ushirikiano katika sekta za nishati, elimu, afya, kilimo, biashara, utalii na uwekezaji.

Tanzania na Namibia zimekuwa na uhusiano wa kihistoria tangu enzi za harakati za ukombozi wa bara la Afrika, na ziara hii inalenga kuimarisha zaidi misingi hiyo ya kihistoria kwa ajili ya maendeleo ya sasa na kizazi kijacho.

Rais Nandi-Ndaitwah pia atatembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria na maendeleo nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kushuhudia maeneo ya uwekezaji na miradi ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Namibia kwa kuendelea kuenzi uhusiano na urafiki kati ya mataifa yetu mawili. Viongozi hao wawili watatoa taarifa kwa vyombo vya habari mara baada ya kumaliza mazungumzo yao rasmi.


No comments:

MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO ATEMBELEA KAMPUNI YA KIMATAIFA YA VIFAA TIBA NCHINI ITALIA

ROMA, ITALIA – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, ametembelea kampuni ya kimataifa ya uzalis...