Friday, May 09, 2025

RAIS WA MSUMBIJI MHESHIMIWA DANIEL CHAPO AWASILI ZANZIBAR KWA ZIARA YA KIKAZI YA KIDIPLOMASIA












Zanzibar, 9 Mei 2025 —
Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mheshimiwa @DanielChapo_ amewasili visiwani Zanzibar kwa ziara rasmi ya kikazi, ikiwa ni mwendelezo wa juhudi za kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania na Msumbiji.

Rais Chapo amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, akitokea Jijini Dar es Salaam, na kupokelewa kwa heshima na makaribisho rasmi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hamza Hassan Juma. Viongozi wengine waliompokea ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, pamoja na maafisa mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika ziara yake, Rais Chapo atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa @DrHmwinyi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, mazungumzo yatakayolenga kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili zinazoshirikiana katika historia, lugha, na malengo ya pamoja ya maendeleo kwa watu wao.

Pamoja na mikutano ya ngazi ya juu, Rais Chapo anatarajiwa kutembelea Kituo cha Uvuvi wa Bahari Kuu kilichopo Fumba, kama sehemu ya kujifunza na kubadilishana uzoefu juu ya matumizi ya rasilimali za bahari kwa ajili ya maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi.

Ziara hii ya Mheshimiwa Rais Chapo ni ishara ya dhamira ya pamoja kati ya Tanzania na Msumbiji ya kuendeleza mahusiano ya kindugu na kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, kilimo, uvuvi, elimu, na afya. 

Aidha, inadhihirisha mshikamano wa kihistoria uliopo kati ya mataifa haya mawili, uliojengwa katika misingi ya ukombozi, mshikamano wa kiafrika, na maelewano ya kisiasa na kiuchumi.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaamini kuwa ziara hii italeta matokeo chanya na kuendeleza mazungumzo ya maendeleo kwa faida ya wananchi wa pande zote mbili.

@NoticiaMoz @opaismz @TVMoz @stvmoz @radiomocambique @AgenciaAIM

#Diplomasia #Zanzibar #TanzaniaMozambique #ChapoInZanzibar

No comments:

MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO ATEMBELEA KAMPUNI YA KIMATAIFA YA VIFAA TIBA NCHINI ITALIA

ROMA, ITALIA – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, ametembelea kampuni ya kimataifa ya uzalis...