Singida, Mei 1, 2025 – Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) mwaka huu yameandika historia mpya nchini Tanzania, baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuongoza maadhimisho hayo kitaifa yaliyofanyika kwa mara ya kwanza katika Viwanja vya Bombadia, mkoani Singida.
Katika shamrashamra hizo, ambazo ziliambatana na maandamano ya amani, hotuba zenye ujumbe wa matumaini, burudani na michezo ya wafanyakazi, Rais Samia alikabidhi zawadi ya vikombe kwa washindi wa michezo mbalimbali iliyoshirikisha timu kutoka taasisi za umma na binafsi, mashirika ya kijamii na vyama vya wafanyakazi.
Michezo hiyo, ambayo ilianza mapema wiki kadhaa kabla ya kilele cha Mei Mosi, ilijumuisha mashindano ya soka, riadha, kuvuta kamba, netiboli na mingine ya kijamii iliyolenga kuimarisha afya, mshikamano na morali ya kikazi miongoni mwa wafanyakazi.
“Michezo ni nyenzo ya kujenga afya bora kwa wafanyakazi na kuongeza mshikamano, nidhamu na morali ya kazi. Serikali itaendelea kuhimiza na kusaidia michezo mahali pa kazi,” alisema Mhe. Rais Samia wakati wa hafla ya kukabidhi vikombe.
Katika kilele cha hotuba yake, Rais Samia alitangaza habari njema kwa wafanyakazi wote wa umma nchini:
“Ninayo furaha kuwatangazia kwamba, mwaka huu Serikali itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1. Nyongeza hii itaanza kutumika mwezi Julai, 2025, ambapo kima cha chini kitaongezeka kutoka shilingi 370,000 hadi 500,000,” alisema kwa msisitizo, na kushangiliwa na maelfu ya wafanyakazi waliokuwa uwanjani.
Aidha, Rais Samia alitumia jukwaa hilo kuwapongeza wafanyakazi kwa uvumilivu na mchango wao mkubwa katika maendeleo ya taifa, na kutoa hakikisho kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kushughulikia changamoto walizozieleza kupitia risala ya TUCTA (Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania).
“Mmeyataja yale yaliyofanyiwa kazi na pia yale yaliyosalia. Serikali haijayapuuza, na tutaendelea kuyashughulikia kwa uzito unaostahili,” aliongeza Rais Samia.
Kauli mbiu ya mwaka huu ilihimiza dhamira ya kitaifa ya maendeleo jumuishi kupitia mazingira bora ya kazi, ikisema:
No comments:
Post a Comment