Dar es Salaam, Mei 5, 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameongoza hafla ya utoaji wa Samia Kalamu Awards 2025, tukio la kipekee linalolenga kutambua mchango wa waandishi wa habari katika maendeleo ya taifa.
Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa The Super Dome, Masaki jijini Dar es Salaam na imehudhuriwa na viongozi wa Serikali, wadau wa sekta ya habari, wanahabari, wanataaluma, na wageni mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Akihutubia hadhira hiyo, Rais Samia aliwahimiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao kama nyenzo ya kujenga taifa lenye mshikamano, uwazi na maendeleo. Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira bora ya kufanya kazi kwa wanahabari kwa kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari unalindwa huku uwajibikaji ukipewa kipaumbele.
"Uandishi wa habari ni moyo wa demokrasia. Kalamu zenu zina nguvu ya kuleta mabadiliko. Tuendelee kushirikiana kwa kuandika habari zenye ukweli, zinazojenga, na zinazohimiza uwajibikaji kwa maendeleo ya taifa letu,” alisema Rais Dkt. Samia.
Katika tukio hilo, Rais Samia alikabidhi tuzo pamoja na mfano wa hundi ya Shilingi milioni 20 kwa Mwandishi wa Habari Mbobevu, Ndugu Tido Mhando, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake mkubwa katika taaluma ya habari nchini.
Tido Mhando alitunukiwa tuzo hiyo kama Mwandishi Mahiri wa Mwaka, kutokana na mchango wake wa muda mrefu katika kukuza weledi wa uandishi na kuibua mijadala muhimu ya kitaifa kupitia vyombo vya habari.
Aidha, Rais alipata nafasi ya kupiga picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo wadau wa habari pamoja na Mwanaharakati maarufu wa haki za wanawake, Mama Getrude Mongella, ambaye pia alihudhuria hafla hiyo kama mgeni wa heshima.
Tuzo za Samia Kalamu Awards zilitolewa katika makundi mbalimbali ikiwemo:
-
Tuzo ya Habari za Uchunguzi
-
Tuzo ya Habari za Mazingira
-
Tuzo ya Habari za Haki za Binadamu
-
Tuzo ya Habari za Maendeleo ya Jamii
-
Tuzo Maalum kwa Mwandishi Mstaafu aliyeacha alama
Tuzo hizi zimeanzishwa kama sehemu ya juhudi za kuhamasisha uandishi wa kiwango cha juu unaozingatia maadili, weledi na uzalendo. Zinatoa motisha kwa waandishi wa habari nchini kuendelea kuibua hoja zenye kuleta tija kwa jamii.
Hafla hiyo pia ilikuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 3 Mei, na imeonyesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuimarisha sekta ya habari kama mhimili wa demokrasia na maendeleo ya taifa.
No comments:
Post a Comment