Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Dkt. Blandina Bugazi Kilama kuwa Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayeshughulikia biashara na ubunifu kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Mei, 2025.
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam, Mei 24, 2025 — Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameongoza hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni kushika nyadhifa muhimu katika Serikali, hafla iliyofanyika Ikulu ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bw. Shaaban Kissu, viongozi waliokula kiapo cha utii na uadilifu mbele ya Rais Samia ni pamoja na Profesa Tumaini Joseph Nagu, aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayesimamia masuala ya afya; Dkt. Blandina Buganzi Kilama, aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayeshughulikia biashara na ubunifu; pamoja na Jaji Mstaafu John Samweli Mgetta, aliyeteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Maadili.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais Dkt. Samia aliwataka viongozi hao kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kwa moyo wa kizalendo. Aliwahimiza kushirikiana kikamilifu na watumishi waliopo katika maeneo yao ya kazi ili kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa kwa ufanisi.
“Ni matumaini yangu kuwa mtaenda kuwa viongozi wa mfano katika maeneo yenu ya kazi. Tekelezeni majukumu yenu kwa bidii, mkiwa watiifu kwa sheria, miongozo na kanuni za utumishi wa umma. Pia zingatieni maadili, nidhamu, na mshikamano na wenzenu kwa manufaa ya Taifa,” alieleza Mhe. Rais Samia.
Aidha, Rais Samia aliwasisitiza viongozi hao kuviishi viapo vyao kwa vitendo kwa kuonyesha uadilifu na uwajibikaji mkubwa katika nafasi walizopewa. Alisema viongozi wa umma wanapaswa kuwa kielelezo cha uongozi bora, wakitoa huduma kwa wananchi kwa haki na usawa, bila upendeleo au urasimu.
Katika hatua nyingine ya hafla hiyo, viongozi walioteuliwa walikula pia kiapo cha maadili ya utumishi wa umma, wakijumuika na viongozi wengine walioteuliwa na kuapishwa katika nyadhifa tofauti. Miongoni mwao ni Dkt. Fred Matola Msemwa, aliyeteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango; Ndugu Lazaro Jacob Twange, Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO); pamoja na Ndugu Thadei Aldo Kabonge, aliyeteuliwa kuwa Msaidizi wa Katibu wa Baraza la Mawaziri.
Uteuzi na uapisho wa viongozi hawa ni sehemu ya juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha utendaji kazi wa Serikali kwa kuweka watu wenye weledi na uaminifu katika nafasi nyeti za uongozi. Viongozi hao wanatarajiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa katika sekta zao husika.
No comments:
Post a Comment