Tuesday, May 27, 2025

TANZANIA NA KOREA KUSINI ZAENDELEZA USHIRIKIANO WA KIDIPLOMASIA KATIKA SEKTA YA ARDHI NA MAKAZI

 














 




Dodoma, Mei 27, 2025 — Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, amekutana na kufanya mazungumzo ya kikazi na Naibu Waziri wa Ardhi, Miundombinu na Uchukuzi wa Jamhuri ya Korea, Mheshimiwa Bw. Jin Hyun Hwan, katika kikao maalum kilichoandaliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mkutano huo umefanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) –  Mkandarasi House Dodoma, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa NHC alikuwa mwenyeji kwa niaba ya wizara, akiwapokea viongozi hao waandamizi na kuwakaribisha katika jengo hilo la kihistoria.

Katika kikao hicho, viongozi hao walijadili kwa kina njia za kuimarisha ushirikiano wa kimkakati baina ya Tanzania na Korea Kusini, hasa katika maeneo ya usimamizi wa ardhi, uendelezaji wa makazi nafuu, na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika upangaji wa miji na utunzaji wa mazingira.

Waziri Ndejembi alisisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania kuhakikisha upatikanaji wa makazi bora na nafuu kwa wananchi, akieleza hatua zinazochukuliwa kupitia miradi kama Samia Housing Scheme, pamoja na mapendekezo ya kushirikiana na Korea katika uboreshaji wa mifumo ya kidijitali ya taarifa za ardhi.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Jin Hyun Hwan alitoa pongezi kwa juhudi za Serikali ya Tanzania na kueleza kuwa Jamhuri ya Korea iko tayari kuendeleza ushirikiano kupitia:

    Mradi wa National Land Data Infrastructure (NLDI) unaolenga kuboresha taarifa za kijiografia na ramani za kitaifa;

    Uendelezaji wa Tanzania Geo-Innovation Center, kituo cha mafunzo ya teknolojia ya ardhi na upimaji kwa kutumia droni na GIS, kinachotarajiwa kuanza rasmi Julai 2025;

    Mafunzo ya kujenga uwezo kwa wataalamu wa Kitanzania kupitia ushirikiano wa kitaaluma na programu za Knowledge Sharing Program (KSP);

    Uboreshaji wa upatikanaji wa vifaa vya ujenzi vya kisasa na rafiki kwa mazingira, kama vile mifumo ya kiyoyozi na vifaa vya ujenzi vinavyotumika nchini Korea.

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Korea Kusini ulioanzishwa mwaka 1992 umeendelea kuimarika kwa miaka, na mkutano huu ni ushahidi wa dhamira ya pamoja kuendeleza maendeleo jumuishi na endelevu yanayozingatia matumizi bora ya ardhi, makazi bora, na teknolojia rafiki kwa mazingira.

No comments:

MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO ATEMBELEA KAMPUNI YA KIMATAIFA YA VIFAA TIBA NCHINI ITALIA

ROMA, ITALIA – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, ametembelea kampuni ya kimataifa ya uzalis...